Kilio cha ubovu wa barabara Tomondo

Unguja. Wakazi wa Tomondo, Mkoa wa Mjini Magharibi wameiomba Serikali kuwajengea miundombinu ya barabara za mtaani kwani ubovu wa miundombinu hiyo, imekuwa sababu ya daladala kukatisha njia na kutofika maeneo yao.

Wakizungumza na Mwananchi Novemba 21, 2024 baadhi ya wakazi wa eneo la Tomondo Mshelishelini, wamesema hulazimika kusafiri kwa bodaboda.

Mkazi wa Tomondo Mshelishelini, Ali Omar Juma amesema tangu kuharibika kwa barabara kwa sasa inafika zaidi ya miaka sita katika eneo hilo na hawana huduma ya usafiri wa umma.

Amesema baadhi ya wajawazito wa eneo hilo wanapata changamoto wanapohitaji kwenda vituo vya afya, kutokana na mtikisiko unaosababishwa na ubovu wa barabara.

“Madereva wa njia hii wamekatisha njia ya daladala za abiria kwa hivyo inatulazimu kutumia usafiri wa bodaboda, wengi wetu tunashindwa kwa sababu kutoka kituo cha daladala hadi tunapofika tunalipia Sh2,000 na hali zetu hizi za maisha ni ngumu na wengine wanatembea kwa miguu,” amesema.

Asma Imran Shaaban amesema barabara hiyo imekuwa kero hususani kwa wagonjwa kwa kuwa kipindi cha jua kali,  usafiri kwa bodaboda huwafanya kushindwa kuhimili.

Halima Yussuf Kombo amesema hali ya barabara hiyo inakatisha tamaa kulinganisha na maeneo mengine ya jirani ambako barabara zimejengwa vizuri.

Dereva anayetumia barabara hiyo, Hamad Majid Saleh amesema baadhi yao hukatisha safari kutokana na ubovu wa barabara wakihofia kuharibu magari yao.

Ofisa Uhusiano Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Hakim Daudi amesema tatizo la kukatisha njia katika eneo hilo lilikwishawasilishwa na wakazi hao na wamekaa na jumuiya zinazohusika na usafiri wa umma kwa lengo la magari hayo kuishia katika maeneo husika.

Akitoa ufafanuzi wa barabara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Makame  Machano amesema wamelipokea ombi hilo kutoka kwa wakazi wa eneo hilo na wizara ina mpango wa kujenga barabara za mjini na vijijini kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wananchi.

Amesema barabara hiyo itajengwa kupitia mradi wa Kampuni ya China,  na kwa sasa ipo katika hatua ya kukamilisha michoro ya barabara hiyo.

Wizara inatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilomita 100.9 chini ya mkandarasi CCECC.

Related Posts