Kocha Muya: Tunarudi tukiwa imara

KUPATA pointi moja katika mechi tatu za mwisho, kumemfanya Kocha wa Fountain Gate, Mohammed Muya kujitafakari huku akisisitiza lazima wafanye jambo.

Fountain Gate ambayo inashika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 17, mechi tatu za mwisho imeambulia sare moja dhidi ya Mashujaa na kupoteza mbili dhidi ya Singida Black Stars na Pamba Jiji.

Timu hiyo inayoutumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara kwa mechi zake za nyumbani, mchezo ujao itaikaribisha JKT Tanzania, Novemba 29 mwaka huu.

“Jambo zuri ni kwamba wachezaji wote wapo vizuri kiafya, matokeo mabaya katika mechi mbili za mwisho ambapo tulitoka sare na kufungwa hayatuvunji moyo, tumejifanyia tathmini na tunawaahidi mashabiki wetu kwamba tutafanya vizuri mechi zinazofuata kumalizia mzunguko wa kwanza,” alisema Muya.

Kazi kubwa aliyonayo Muya ni kuhakikisha katika mechi nne zijazo za kukamilisha mzunguko wa kwanza dhidi ya JKT Tanzania (nyumbani), Coastal Union (nyumbani), Azam (ugenini) na Yanga (ugenini) ni kutopoteza pointi kirahisi.

Fountain Gate imeonekana kuwa na shida kubwa eneo la ulinzi kutokana na kuruhusu mabao 20 sawa na KenGold ambapo timu hizo ndizo zimeruhusu mabao mengi zaidi.

Licha ya kwamba ulinzi kuna tatizo, lakini Muya anajivunia safu yake ya ushambuliaji iliyofunga mabao 20 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Simba yenye 21, huku mshambuliaji wao, Seleman Mwalimu akiongoza kwa mabao sita.

Related Posts