LHRC: Wagombea serikali za mitaa jengeni hoja, acheni vihoja

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimewataka wagombea wa vyama vyote kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kujikita katika hoja zenye kujenga na wananchi kutumia kampeni kuchagua kwa busara viongozi bora kwa miaka mitano ijayo.

Kampeni za uchaguzi huo zilianza Novemba 20, 2024 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, kwa kuwachagua wenyeviti na wajumbe wa kamati za mitaa katika miji, vijiji na vitongoji.

Akizungumza leo, Novemba 22, 2024, Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa LHRC, Fulgence Massawe amesisitiza umuhimu wa amani, utulivu na mshikamano kabla, wakati na baada ya uchaguzi huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura.

Massawe amesema hayo wakati wa mafunzo kwa waangalizi wa uchaguzi kuhusu maadili, sheria, kanuni za uchaguzi, na masuala mtambuka yaliyoandaliwa na kituo hicho.

Waangalizi hao watafuatilia mwenendo wa uchaguzi ili kuhakikisha kama ni huru, haki na wa uwazi, na taarifa zao zitatumika kuandaa mapendekezo kwa Ofisi ya Rais – Tamisemi.

LHRC, iliyopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuatazama uchaguzi huu, inalenga kutoa taarifa sahihi na kusaidia maboresho ya chaguzi zijazo.

Catherine Michael, mshiriki wa mafunzo hayo, amesema yatawawezesha kukusanya taarifa sahihi na kusaidia jamii kwa kutoa taswira ya kweli ya uchaguzi na manufaa yake kwa wananchi.

Related Posts