Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema somo la biashara litakuwa ni lazima kwa wanafunzi wote kuanzia mwaka wa masomo 2025/26, kwa lengo la kujenga kizazi chenye kufikiri kwa mrengo wa kibiashara zaidi.
Amesema hayo leo Ijumaa Novemba 22, 2024 alipofungua kongamano la tano la maendeleo ya biashara na uchumi lililoandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
“Serikali kwa upande wetu kupitia Sera ya Mafunzo ya mwaka 2023 inaelekeza somo la biashara liwe la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026 na kuendelea,” amesema.
Amesema hiyo ni fursa kwa vyuo vya elimu ya biashara kuanzisha na kuendeleza kozi za muda mfupi na mrefu kwa walimu, ili kufikia malengo ya taaluma ya elimu ya biashara nchini.
Majaliwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha mtalaa wa elimu ya biashara kwa ngazi ya sekondari, kwa lengo la kuandaa vijana kuwa na msingi na ujuzi wa biashara.
“Lengo hapa ni kuwawezesha wahitimu wa ngazi ya sekondari kuchangia kwa ufanisi uchumi wa Taifa, kupitia mtalaa huu tunatarajia kujenga kizazi chenye uwezo wa kufikiri kibiashara zaidi, lakini kutumia fursa zilizopo kwa kuanzisha miradi mbalimbali,” amesema.
Majaliwa ameviagiza vyuo kuhimiza wataalamu kufanya utafiti na kuendelea kufanya tafiti na kutumia matokeo yake kuboresha mbinu za utengenezaji bidhaa zenye masoko.
Amevitaka vyuo vya elimu ya biashara kuweka mkazo katika umuhimu wa kutoa elimu ya maadili ya biashara, ili kuwezesha kuwa na uwazi na uwajibikaji katika kufanya biashara.
“Hata kama biashara ni ya mtu binafsi ni muhimu wakajua namna ya uwajibikaji katika kufanya biashara. Ukijua kuwa unalipa kodi lazima ujijengee nidhamu katika kufanya biashara, wawe na muda wa kufungua na kufunga biashara zao,” amesema.
Amesema watakapotengeneza mitalaa, jambo hilo liwe sehemu ili wahitimu wakatekeleze ili kuondokana na tabia zisizofaa katika biashara.
“Wasomi wetu wa sekta ya biashara mko hapa zingatieni mtalaa ili kila mmoja anapomaliza masomo afikirie zaidi kufanya biashara kuliko kusubiri kuajiriwa na Serikali.
“Serikalini nafasi zimejaa, wengi ni vijana wana miaka 30 na ili atoke hapo ni awe na miaka 60, kwa hiyo kuna miaka mingine 30 ya kusubiri,” amesema.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema majukumu makubwa ya CBE, ni kuhakikisha wanatengeneza mazingira ili watu wapate ajira.
Amesema kwa takwimu za mwaka 2021, wahitimu wa vyuo vikuu walikuwa 51,800 lakini mwaka 2022 wameongezeka na kuwa 64,000.
“Mwaka huu wanakadiriwa watafika kati ya 69,000 hadi 70,000 ambao hawawezi kuajiriwa na Serikali. Idadi kubwa ya vijana hawa tunategemea waende wakaajiriwe katika sekta binafsi. CBE inatengeneza mazingira jinsi gani watu waweze kujiingiza na kufahamu biashara,” amesema.
Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga amesema wamekuwa wakiwapatia elimu ya biashara makundi yasiyo rasmi ili kuwawezesha kuwa rasmi.
Amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), wameandaa mtalaa kuwafundisha wahudumu wa mabasi yanayokwenda masafa marefu.
“Tulitengeneza mtalaa ukathibitishwa na sasa tumeshafundisha wahudumu wa mabasi 45, imesaidia wanapomaliza kupata certificate (cheti) na kusajiliwa na Latra. Inaweza kusaidia kupata ajira,” amesema.
Amesema mwaka jana walitoa elimu kwa madalali wa mali zisizohamishika wakishirikiana na Chama cha Madalali Tanzania, hivyo kupata cheti na kuwa rasmi.
Profesa Lwoga amesema Novemba, mwaka huu wamesaini makubaliano na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), ili kuvijengea uwezo vyama vya ushirika vifanye kazi kibiashara zaidi.
Mkataba huo amesema utawezesha kuvifikia vyama vya ushirika zaidi ya 7,000.
Akijibu swali bungeni la Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina Februari 3, 2023, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema asilimia 12.2 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 35 nchini Tanzania hawana ajira.
Alisema idadi hiyo ni sawa na vijana milioni 1.73 kati ya nguvu kazi ya vijana milioni 14.21 wenye uwezo wa kufanya kazi