Dar/Mikoani. Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji zikiingia siku ya tatu leo Novemba 22, 24 vyama vikinadi sera, baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekamatwa na polisi mkoani Songwe.
Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 zilianza Novemba 20 na zitahitimishwa Novemba 26.
Polisi Mkoa wa Songwe limesema linawashikilia viongozi hao akiwamo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kwa mahojiano baada ya kukiuka utaratibu wa kampeni.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 22, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agustino Senga amesema: “Ni kweli tunamshikilia Mbowe na viongozi wengine japo idadi yao bado sijaipata kwa mahojiano zaidi kutokana na kukiuka utaratibu wa kampeni.
“Aliposhuka uwanja wa ndege alipopokewa na kusalimia kisha akataka kuweka na mkutano papohapo jambo ambalo si sahihi kwa kuwa vyama vyote viliwasilisha maeneo ya mikutano yao.”
Ametoa rai kwa vyama vyote kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi akieleza Jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwenda kinyume hasa kipindi hiki.
Mbowe yuko mkoani humo kufungua kampeni za chama hicho akianzia Mlowo, Vwawa kisha Mji wa Tunduma kabla ya kesho Jumamosi Novemba 23 kuelekea mkoani Mbeya.
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Songwe, Isakwisa Lupembe amedai kiongozi wao amefanyiwa vurugu walipotawanywa wananchi.
“Wanatawanywa wananchi kwa mabomu na kuleta taharuki kwa waliofika kumsikiliza kiongozi wetu, tunachokibali cha kampeni inakuwaje tunazuiwa, tunataka haki itendeke,” amesema.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema imesema katika Pori la Halungu wilayani Mbozi msafara wa chama hicho ulivamiwa na polisi waliomkamata Mbowe na viongozi alioambatana nao.
Amesema Mbowe alishafanya mikutano ya kampeni katika Kata ya Itaka, Kijiji cha Itewe na Kata ya Halungu Mjini.
Mrema amesema mkutano wa kwanza uliokuwa ufanyike mji wa Mlowo ulizuiwa na polisi ambao Chama cha ACT-Wazalendo kiliwaalika Chadema kushiriki. Amesema Polisi walikataa na kutawanya wananchi kwa mabomu ya machozi.
Kwa mujibu wa Mrema viongozi wa Chadema kabla ya kukamatwa walifuatwa na gari ya Polisi ambao waliwashusha kwa nguvu kwenye magari na kuwashambulia.
Mbali na Mbowe, wengine waliokamatwa ni Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mwenyekiti Kanda ya Nyasa), Pascal Haongo (aliyewahi kuwa mbunge wa Mbozi Mashariki), Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Wilaya ya Mbozi, Appolinary Boniface (Mkuu wa Digital Platform), Paul Joseph (Ofisa Habari Kanda ya Nyasa), Calvin Ndabila (Ofisa Habari Kanda ya Nyasa), Mdude Nyagali (Mwanaharakati na mwanachama wa Chadema), wasaidizi wa Mbowe ambao ni Bwire, Adamoo na Lingwenya.
Chadema imelaani kukamatwa kwa viongozi hao ikitaka waachiwe bila masharti ili waendelee na ratiba ya mikutano ya kampeni.
Jana, Novemba 21, 2024, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu alizuiwa na polisi kufanya mkutano katika Kata ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Semu ambaye amejikita kufanya kampeni katika ukanda wa Pwani na mikoa ya kusini akiwa na msafara wake walizuiwa ikidaiwa ni kwa amri ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD).
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Protas Mutayoba alisema kwa mujibu wa ratiba waliyonayo chama hicho hakikupangiwa kufanya kampeni katika eneo hilo, ndiyo maana walizuia na kuwatawanya kwa amani.
“Jeshi la Polisi linatoa rai kwa vyama vya siasa na wagombea kuzingatia ratiba za kampeni badala ya kujipangia ratiba zao tofauti kwa visingizio vyovyote. Kama wanasababu za kubadili ratiba basi wawasiliane na msimamizi wa uchaguzi,” alisema Kamanda Mutayoba katika taarifa kwa umma.
Rais Samia Suluhu Hassan kwa nyakati tofauti amekuwa akisema mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakuwa huru na haki.
Kwa upande wake, Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amekuwa akisema mchakato wa uchaguzi utasimamiwa kwa falsafa ya 4R (maridhiano, ustahimilivu, kujenga upya na mageuzi), akivitaka vyama kuheshimu taratibu zilizowekwa.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema watapiga kampeni hata maeneo ambayo wagombea wao wote wamekatwa ili kufundisha wananchi cha kufanya.
Amesema wagombea wa chama hicho zaidi ya asilimia 70 katika kanda hiyo walienguliwa lakini hilo halijawakatisha tamaa bali wanajifunza nini cha kufanya katika uchaguzi ujao wa madiwani, wabunge na Rais.
Lema alisema hayo jana Novemba 21, kwenye uzinduzi wa kampeni ya wagombea wa viongozi wa serikali za mitaa Kanda ya Kaskazini iliyofanyika katika viwanja vya stendi ya Kilimbero jijini Arusha.
“Hata waengue wote abaki mmoja tutapiga kampeni kote, mnaweza kujiuliza tunaenda kuwaambia nini wananchi tena maeneo ambayo hatuna wagombea, niwaambie nitakwenda siyo kwa sababu ya kushinda uchaguzi bali nitakwenda kuwafundisha hatua muhimu za kuchukua dhidi ya watawala,” amesema.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema chama hicho, kitaheshimu na kuzingatia ratiba zote za kampeni zilizowekwa na mamlaka husika, akiwataka viongozi na watendaji wa CCM kwenye ngazi zote kuonyesha mfano wa kuheshimu.
Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ameeleza hayo leo Novemba 22 alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Msichoke, Vingunguti.
“Nasema hili hadharani kwa sababu kule Songwe kuna chama kimekurupuka, kimekwenda kulikuwa na ratiba ya Chama cha ACT-Wazalendo, lakini wao walikwenda na kutaka kufanya mkutano, kukatokea fujo.
“Sitaki kukisemea hicho chama, lakini nimeona nisema CCM hatutakuwa kama wao wa kutoheshimu ratiba za kampeni, bali sisi tutakuwa chama kiongozi cha kuheshimu kampeni,” amesema.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ikitoa mikopo yenye thamani ya Sh141.8 milioni kwa vikundi 10 vya vijana na wanawake, Mkuu wa wilaya hiyo, James Kaji ametumia nafasi hiyo kuiombea CCM kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Mikopo hiyo ambayo ni ya kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25, ilikabidhiwa jana Novemba 21, 2024 kwa vikundi sita vya wanawake na vinne vya vijana.
Akikabidhi mikopo hiyo, katika ofisi za halmashauri hiyo, Kaji aliwaasa wanavikundi hao kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kuyafikia malengo na kuzirejesha kwa wakati.
Hata hivyo, aliwataka wananchi hao kuwa na shukrani kwa CCM na kuichagua Novemba 27, katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Niwaombe katika hiyo mikopo, mkaitumie vizuri, fanyeni kwa uadilifu na Mungu atawasaidia ili mkirudisha na wengine wapate, nendeni mkafanye miradi mliyoomba na mkiona mnakwama, rudini kuomba ushauri wa kitaalamu.
“Pia nawashukuru wabunge lakini kabla ya wabunge Chama cha Mapinduzi ambacho kinajali wananchi, sasa mnapewa mikopo hii, muende kule kwingine shauri yenu kama mtakuja kupata tena, muwe na shukrani, tunakwenda kwenye uchaguzi, kwa hiyo niwaombe kwenye uchaguzi chagueni CCM.”
Wilayani Kibaha, mkoani Pwani wananchi wamekumbushwa kuwa kukosekana wagombea wa upinzani kwenye baadhi ya mitaa hakuwezi kuwa sababu ya kuwapa ushindi wagombea wao, badala yake kitakachowafanya washinde ni kujitokeza kupiga kura.
Akimnadi mgombea wa uenyekiti wa Kitongoji cha Mwembe Baraza, Kibaha kwa tiketi ya CCM, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa ushindi unapatikana kwa wingi wa kura, hivyo wajitokeze kupiga kura Novemba 27.
Mgombea wa nafasi hiyo, Anna Mwakyusa amesema anatambua changamoto zilizopo kwenye eneo hilo kwa kuwa awali alikuwa mmoja wa wajumbe wa serikai ya mtaa huo, hivyo anajua anachokwenda kufanya.