Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe pamoja na Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Nyassa Joseph Mbilinyi (Sugu) wanashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani Songwe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Songwe … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema imeeleza kuwa, Viongozi hao na baadhi ya wanachama na watumishi wa chama hiko, walikamatwa mara baada ya kufanya mikutano ya kampeni kwenye Kata ya Itaka, kijiji cha Itewe na Kata ya Halungu Mjini.

Taarifa ya Chadema haikueleza sababu maalum za kukamatwa kwa viongozi na wanachama wao, ambapo kwa mujibu wa taaifa iliyotolewa na katibu Mkuu wa Chama hiko John Mnyika kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa ‘X’ zamani Twitter aliandika kuwa mara baada ya kukamatwa walipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Vwawa.

Viongozi hao wa Chadema wamekamatwa, wakiwa kwenye siku ya kwanza ya ufunguzi wa kampeni kuelekea uchaguzi wa Serikali za kitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024, kwa majimbo majimbo yote ya mkoa wa Songwe.

Aidha Chama hiko kimelaani kitendo hiko cha kukamatwa kwa Mbowe na wanachama wengine, na kimesema kuwa huo ni mkakati wa kuhujumu kampeni za Chama chao kwa vyombo vya Dola kushirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika hatua nyingine Chadema imelitaka jeshi la Polisi mkoani Songwe, kuwaachia mara moja bila masharti yoyote makada wao ili waweze kuendelea na kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Wengine waliokamatwa katika tukio hilo ni Pascal Haongo, Mbunge wa zamani wa Mbozi Mashariki, Appolinary Boniface mkuu wa Digital Chadema, Paul Joseph Afisa Habari Kanda ya Nyassa, Mdude Nyagali na Bwire, Adamoo na Lingwenywa ambao ni wasaidizi Mbowe.

About The Author

Related Posts