NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa viti maalum mkoani Kilimanjaro, Zuena Bushiri amewanadi wagombea wa mtaa wa Kiusa laini na Kiusa sokoni kata ya Kiusi manispaa ya Moshi ambapo ndipo kata ya nyumbani ya Mbunge huyo.
Zuena alisema kuwa, zipo sababu za wananchi wa kata hiyo ya Kiusa kuwachagua wagombea wanaotokana na chama cha Mapinduzi kwani kazi kubwa wameweza kuifanya ya kuwatumikia wananchi kwa miaka mitano iliyopita.
“Wapo wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakipita na kuwadanganya kuwa kipindi cha miaka mitano hakuna kilichofanyika msidanganyike ninyi ni mashahadi kazi nyingi na kubwa zimeweza kufanyika” Alisema Mbunge Zuena.
Mbunge huyo alisema kuwa, serikali ya Chama cha Mapinduzi imetoa fedha nyingi katika kata hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwaomba wananchi kukilipa chama hicho kwa kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM.
Katika hatua nyingine Mbunge huto aliwaomba wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la mkazi kutumia haki yao ya kupiga kura Novemba 27 mwaka huu na kuwachagua viongozi bora ambao wanatokana na chama cha Mapinduzi.
Aidha Mbunge huyo alipita katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo ikiwemo kwenye magereji na maeneo mbalimbali ya biashara huku akiwanadi na kuwaombea kura mgombea wa Uenyekiti mtaa wa Kiusa sokoni, Salma Kabwe na Mwenyekiti wa mtaa wa Kiusa Laini, Julius Raymond.