Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limesema bado linaendelea na uchunguzi wa matukio mawili yaliyojitokeza nchini, likiwemo lile la mfanyabiashara Deogratius Tarimo aliyenusurika kutekwa na watu waliojitambulisha kuwa ni askari eneo la Kiluvya, jijini Dar es Salaam.
Mbali na tukio hilo, lingine ni lile linalohusu mmiliki/wamiliki wa jengo lililoanguka Kariakoo Novemba 16, 2024 na kusababisha madhara vikiwemo vifo vya watu 20 na majeruhi zaidi ya 80.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 22 na Jeshi hilo kupitia kwa Msemaji wake, David Misime, uchunguzi wa matukio yote mawili umefikia katika hatua nzuri.
“Upelelezi wa kesi hizi mbili upo katika hatua nzuri na hivi karibuni taarifa kamili itatolewa kwa umma,” amesema Misime.
Misime amesema wamelazimika kutoa taarifa hiyo kwa kuwa wamekuwa wakipokea maswali na maoni mengi kutoka kwa waandishi wa habari na wananchi kutaka kufahamu.
“Kumekuwepo na maswali na maoni mengi kutoka kwa waandishi wa habari na wananchi wakitaka kufahamu hatua iliyofikiwa ya matukio hayo mawili,” amesema taarifa hiyo.
Novemba 11, 2024, katika hoteli ya Rovenpic iliyopo maeneo ya Kiluvya Madukani, Tarimo alinusurika kutekwa.
Picha za video za tukio hilo zilianza kusambaa mitandaoni Novemba 12, zikiwaonyesha watu watatu wakimlazimisha mfanyabiashara huyo kuingia katika gari bila mafanikio na baadaye kuamua kumuacha.
Novemba 13 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa umma kwamba lilikuwa limeanza uchunguzi wa tukio hilo.
Kuporomoka kwa jengo Kariakoo
Katika hatua nyingine, baada ya kuporomoka kwa jengo la Kariakoo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa Jeshi la Polisi kumkamata mmiliki wa jengo hilo.
“Naagiza mmiliki wa hili jengo atafutwe popote alipo akamatwe aje atueleze kwa nini jengo hili limeanguka na ataeleza mbele ya Kamati ambayo imeundwa ya uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Majaliwa Novemba 18 mwaka huu.