Akilihutubia taifa lake kwa njia ya televisheni jioni ya jana, Rais Vladimir Putin wa Urusi ametangaza kuwa Urusi imetumia aina mpya ya kombora la masafa ya kati, kushambulia kituo cha kijeshi cha Ukraine. “Wataalamu wetu wa makombora waliliita Oreshnik. Majaribio yalifanikiwa. Lengo la uzinduzi lilifikiwa. Moja ya majengo makubwa na maarufu zaidi ya kiviwanda tangu enzi za Umoja wa Kisovieti ambayo bado huzalisha makombora na silaha nyingine leo liliharibiwa kwenye eneo la Ukraine katika jiji la Dnepropetrovsk (Dnipro).”
Awali Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alikuwa amesema kuwa shambulizi la Urusi lilitumia makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kuvuka bara, maarufu kama ICBM. Ukraine haikutoa maelezo zaidi juu ya shabaha iliyolengwa na Urusi wala kiwango cha uharibifu uliotokana na shambulizi hilo.
Katika hotuba yake Putin alidai hatua ya jeshi la Urusi ilikuwa jibu kwa uamuzi wa Marekani na Uingereza kuiruhusu Ukraine kushambulia maeneo ya ndani ya Urusi kwa kutumia makombora ambayo nchi hizo zimeipatia Ukraine.
Aidha, Putin ameongeza kuwa Urusi inayo haki ya kulipiza kisasi dhidi ya nchi ambazo silaha zao zitatumiwa na Ukraine kushambulia ardhi ya Urusi. Ameongeza kuwa kilichoanza kama mzozo wa kivita wa kieneo, kimepanuka na kuchukua sura pana ya kidunia. “Wakiendelea na mzozo wa Ukraine unaochochewa na nchi za Magharibi, Marekani na washirika wake wa NATO walitangaza hapo awali kwamba wanatoa ruhusa ya kutumiwa makombora yao ya masafa marefu na yenye usahihi wa hali ya juu katika maeneo ya ndani ya Urusi. Wataalam wanafahamu vyema, na upande wa Urusi umesisitiza mara kwa mara hili, kwamba haiwezekani kutumia silaha hizo bila ushiriki wa moja kwa moja wa wataalam wa kijeshi kutoka nchi zinazozalisha silaha hizo.”
Katika joto hili la mvutano huu linalozidi kupanda, Volodymyr Zelensky amewataka Waukraine kuendelea kuwa watulivu na kuepuka kusambaza hofu wakati Urusi ikizidisha shinikizo la mashambulizi makali ya anga.
Kulingana na Rais Putin, kombora jipya lililotumiwa na Urusi kuishambulia Ukraine linajulikana kama Oreshnik, ama rangi ya khaki. Urusi hali kadhalika imeyadungua makombora mawili ya Storm Shadow yaliyotengenezwa nchini Uingereza, bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote.
Katika mwendelezo huo wa uhasama, Marekani imeweka vikwazo dhidi ya Gazprombank, benki ya tatu kwa ukubwa nchini Urusi. Vikwazo hivyo vinayahusu pia matawi sita ya Gazprombank.
Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen alisema vikwazo hivi vinakusudia kudhoofisha juhudi za kijeshi za Urusi kwa kuzuia uwezo wake wa kukwepa vikwazo vilivyopo na kununua vifaa vya kijeshi.
afp, ap, reuters, dpa