RC Mtanda ajibu tuhuma za Simba, ambana Ahmed Ally

Baada ya Klabu ya Simba kutoa taarifa jana kwa umma ikilaani kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kuvamia mazoezi ya mwisho ya timu yao na kuwakamata Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu na Kocha Msaidizi, Seleman Matola, kiongozi huyo amekanusha madai hayo.

Mtanda ameziita tuhuma hizo za Simba dhidi yake kuwa ni propaganda zinazosambazwa kutuliza upepo wa mchezo wa Pamba Jiji dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa 0-1.

Jana Alhamisi Novemba 21, 2024, Mpiga picha wa Simba, Rabbi Hume alichapisha kipande ‘Clip’ cha video kwenye ukurasa wake wa Instagram kikionyesha mvutano wa watu kwenye geti kuu la kuingia ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba huku vurugu hizo zikitajwa kuwa ni viongozi wa Simba wanakamatwa na watu aliyodai wametumwa na RC Mtanda.

Baadaye Simba ilitoa taarifa kwa umma na kudai kuwa imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana vilivyofanywa na viongozi wa timu ya Pamba Jiji kwa kushirikiana na mkuu huyo wa mkoa kwa kutumia askari polisi huku ikilaani matumizi ya vyombo vya dola katika mpira wa miguu.

Kufuatia tuhuma hizo, leo Ijumaa Novemba 22, 2024, RC Mtanda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo ameitisha mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo na kukanusha kuihujumu Simba huku akidokeza kuwa amejikuta mwathiriwa wa kitendo hicho kwa kuwa ni mlezi wa Pamba Jiji.

“Hapa CCM Kirumba Pamba ameshacheza mechi nyingi mmeona timu yoyote ikihujumiwa kwanini itokee kwa Simba lakini pia hata Yanga itakuja hapa mimi najua timu kubwa zinapokuja hapa ni lazima hizi kelele za namna hii zitajitokeza. Sisi tumepandisha timu ya Pamba ili hizi timu kubwa zije hapa kwa hiyo ni lazima tuzipokee kwa ukaribu,” amesema Mtanda.

Ameongeza kuwa. “Unajua ni vitu vya kuchekesha timu ya Simba pale walipolala Isamilo nimepeleka askari na doria ifanyike asubuhi mpaka usiku ili waishi na waondoke hapa wakiwa salama, nina haja gani ya kwenda kufanya hujuma ya waziwazi wakati ninao uwezo wa kufanya hujuma ya chinichini na mtu yeyote asione. Mimi ni kiongozi mwenye uzoefu na sina upeo mdogo wa kufanya mambo ya kipumbavu.”

Mtanda amesema akiwa kiongozi kinara wa mkoa huo hawezi kuchafua taswira nzuri ya Mwanza huku akizihakikishia timu zote bila kujali ukubwa wa jina kuwa atazipa ushirikiano kwa sababu anaamini mpira ni dakika 90 huku akisisitiza kuwa mambo hayo ya nje ya uwanja ni kuwaandaa watu kisaikolojia waone kwamba timu inafanyiwa fujo lakini uhalisia hauko hivyo.

Akizungumzia kuhusu hatua atakazozichukua dhidi ya Meneja Habari wa Simba Ahmed Ally kwa madai kuwa amemchafua, Mtanda amesema ameshamsamehe na tayari amewasiliana na mmoja wa viongozi wa Simba na kuomba radhi huku akidai yuko tayari kuwajibika kama endapo kamati ya maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itabaini ametenda kosa.

“Mimi mwenyewe hata kamati ya maadili ya TFF wakifanya uchunguzi wakaona nimehusika kwa namna moja au nyingine kutotimiza wajibu wangu au kuingilia shughuli zao wapo tayari kunichukulia hatua kwa sababu wanaruhusiwa wana kanuni za maadili na mimi nilishakuwa mwenyekiti wa hiyo kamati,” amesema Mtanda na kuongeza.

“Hakuna kitu ni propaganda tu ni uongo umetengenezwa kuchafua watu na kuhamisha attention ya watu wengine wanasema ‘game mind’ kuwafanya watu watoke kwenye mchezo lakini uhalisi hauko hivyo,”

Mtanda amesema klabu hiyo haina uadui na Simba kwani tayari kuna mawasiliano wamefanya kwa kuandika barua kuiomba Simba wachezaji wawili kwa mkopo katika dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15, mwaka huu.

“Mimi ni mwanasiasa na kiongozi ni mlezi nilikuwa naongea na Salim Abdallah ‘Try Again’ hapa na ameniomba radhi kwa tukio hili lote ambalo limetokea lakini mimi nikamwambia hana haja ya kuniomba radhi kwa sababu mimi na uongozi wa Simba tuna mahusiano mazuri ila hawa vijana pengine wakishaona wamekuwa maarufu wanafikiri kwamba wanaweza kuvunja heshima kwa kila mtu,” amesema.

Ameongeza kuwa “Na sisi Simba tuna ugomvi nao gani hata klabu yetu ya Pamba imeandika barua ya kuomba wachezaji wawili kwa mkopo kutoka Simba tungekuwa hatuna mahusiano mazuri tungewezaje kupeleka barua zetu.

“Lakini jambo la kuweka wazi mimi naamini ukweli unaishi, unadumu, kwa hiyo ukweli baada ya hiyo mechi yote haya yataisha,” amesema Mtanda.

Pamba ilikuwa kibaruani leo dhidi ya Simba, mchezo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa 0-1 Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

Related Posts