Mwishoni mwa wiki iliyopita eneo la Kariakoo lenye shughuli nyingi za biashara, kulitokea ajali ya kuanguka kwa jengo la ghorofa nne na kusababisha vifo vya watu takribani 20 na majeruhi zaidi ya 70. Watoa huduma za dharura na uokoaji, vyombo vya ulinzi na usalama, watu wanaojitolea ni moja ya makundi ambayo usiku na mchana waliendelea kutafuta watu waliokwama katika jengo hilo.
Kwa kawaida, jengo linapoanguka hutawanyisha vitu vizito, zikiwamo kuta, mawe, vyuma, mbao, vioo, vibanzi, vumbi la mchanga na saruji.
Sababu za watu kufariki dunia mapema katika eneo la ajali ni pamoja na kuangukiwa na kuta au vitu vizito, kuchomwa na vitu vyenye ncha kali, vumbi linapotimka husababisha waathirika kuvuta hewa yenye vumbi au njia ya kinywa kuingia vumbi na vumbi lile huziba njia ya hewa.
Pia kukwama katika eneo lenye hewa kidogo, mwili kuishiwa nguvu kutokana na kukaa muda mrefu bila kula chakula na kunywa maji, kupatwa na mstuko wa mwili na maumivu makali.
Ustahimilivu wa mwili kuweza kuishi katika eneo lenye hewa finyu linatofautiana kati ya mtu na mtu. Mfano wapo ambao miili yao ina ustahimilivu wa kuendelea kuishi katika hewa ndogo muda mrefu.
Katika hali ngumu kama ile, wanawake wana ustahimilivu zaidi kuendelea kuishi bila kula na kunywa maji kwa muda mrefu kuliko wanaume. Hii inatokana kuwa kiasili mwanamke kuwa na akiba kubwa ya maji na nguvu (mafuta) mwilini.
Vifo vya baadaye vinaweza kujitokeza kutokana na kupata majeraha mengi mwilini, majeraha ya kichwa, ogani kujeruhiwa na kushindwa kufanya kazi na damu kuvuja ndani kwa ndani hasa maeneo ya tumboni.
Maeneo ya mwili ambayo yakijeruhuwa yanachangia vifo ni pamoja na kichwani (ubongo), njia ya hewa, moyo na mishipa mikubwa ya damu na uti wa mgongo.
Majeraha ambayo yanajitokeza mara kwa mara katika ajali ya kuanguka kwa majengo ni pamoja na tishu laini kupata mkatiko, mchaniko, michubuko, mivunjiko ya mifupa, majeraha ya viungo ndani ya tumbo, uti wa mgongo na kujeruhi njia ya hewa.
Vilevile majeraha ya kuungua, kupigwa na umeme na kugusana moja kwa moja na kemikali sumu.
Uwepo wa vifo na majeruhi wengi hutegemeana na aina ya jengo, mazingira ya jengo lilipo, aina ya majeraha, muda wa kupata huduma ya kwanza au ya dharura, eneo alipo muathirika na uwepo wa hewa.
Mambo mengine ni utayari kwa haraka kwa huduma za dharura, majanga na maafa, ujuzi wa kukabiliana na majanga na maafa, vifaa na zana za kuokolea, ujuzi na ufahamu wa jamii kutoa msaada wa dharura, uwezo wa mfumo wa huduma za afya kuhudumia majeruhi na wagonjwa wa dharura.
Lakini pia kuweza kustahimili na kunusurika kifo katika eneo la janga, kutegemea pia na hali ya mwili, umri, uwepo wa magonjwa mengine mwilini.
Mfano mtu anaweza akawa hajapata majeraha yoyote lakini kishindo cha ghafla kinaweza kumsababishia kupata mshtuko wa moyo au kupata shinikizo kubwa la ghafla la moyo.
Ni muhimu kila mwanajamii kujifunza au kuzingatia mafunzo ya utoaji huduma ya kwanza, dharura na uokoaji ili kuweza kusaidia kutoa huduma pale linapotokea janga.