Dar es Salaam. Shahidi wa pili wa upande wa mashtaka katika kesi ya kuwepo nchini bila kibali, inayomkabili raia wa Burundi, Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu kama Chuma cha Chuma, ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo alipewa viza ya matembezi ya siku 60.
Hata hivyo, kibali hicho kilipokwisha muda wake hakurejea Uhamiaji kuomba kuuhisha kama sheria inavyotaka.
Shahidi huyo Patrick Kiondo (45), ambaye ni Mkaguzi kutoka Idara ya Uhamiaji, Kitengo cha Upelelezi Kinondoni, ametoa ushahidi wake leo, Novemba 22, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Chuma, ambaye ni msanii wa muziki na mkazi wa Mbezi Louis, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 4, 2024 na kusomewa shtaka hilo.
Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Raphael Mpuya mbele ya Hakimu Yusto Ruboroga, shahidi amedai kuwa Oktoba 21, 2024 mshtakiwa alipelekwa ofisi za Uhamiaji Kinondoni akitokea Kituo cha Polisi Oysterbay.
“Tulimpokea pale kituoni kwetu akiwa na barua na hati yake ya kusafiria” amedai Kiondo na kuongeza.
“Tulichukua maelezo yake na nilibaini mshtakiwa alikuja nchini mwaka 2021 kwa ajili ya kukutana na mwenzake ambaye ni raia wa Urusi (Russia) na wakasafiri kwenda Zanzibar.”
Hata hivyo, Kiondo ameeleza kuwa baada ya hapo alirudi nchini kwao Burundi na mwaka 2022 alirejea nchini Tanzania na kupewa viza ya matembezi ya siku 60.
“Katika mahojiano na mshtakiwa, nilibaini mshtakiwa aliishi nchini kinyume cha sheria kwa sababu viza yake iliisha muda Agosti 11, 2022.
Amedai barua ya polisi ilionyesha kuwa raia huyo wa Burundi alikamatwa Septemba 18, 2024 akiwa na makosa ya kuwepo nchini kinyume cha sheria.
“Desemba 9, 2020 mshtakiwa huyu alikamatwa kwa kosa kama hili na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita na aliambiwa afuatilie vibali vya kuishi nchini, lakini hakufanya hivyo.”
Shahidi pia ameomba hati hiyo ya kusafiria iingizwe mahakamani na kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.
Baada ya kutoa ushahidi huo, mshtakiwa alipata nafasi ya kumuuliza maswali shahidi na ifuatavyo ni sehemu ya mahojiano.
Mshitakiwa: Kwanza namshukuru Mungu nina miaka miwili sijaigusa wala kuiona pasipoti yangu, naomba niiguse.
Hakimu: Muulize maswali shahidi.
Mshtakiwa: Je, mlinipeleka ofisi ya Uhamiaji mara ngapi? Na kwanini mlinihoji bila kuwa na Pasipoti yangu?
Shahidi: Mheshimiwa hakimu mara ya kwanza tulikataa kumhoji kwa sababu hakuwa na hati ya kusafiria, lakini mara ya pili alipoletwa ofisini kwetu akiwa na pasipoti ndipo tilipomuhoji.
Baada ya mshtakiwa kumaliza kumhoji shahidi, upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake na Hakimu Ruboroga alihirisha kesi hiyo hadi Novemba 25, 2024 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Chuma, ambaye makazi yake ya muda ni Mbezi Lousi na makazi ya kudumu Burundi, anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 18, 2024 alipokutwa eneo la Upanga, Las Vegas Casino, Ilala, Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa akiwa eneo hilo, alibainika kuwepo nchini bila kibali, wakati akijua ni kinyume cha sheria.