TANZANIA NA CHINA ZASISITIZA KUKUZA USHIRIKIANO

Serikali ya Tanzania na China zimesisitiza kuongeza ushirikiano wa kimaendeleo kupitia ziara mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa juu wa pande zote mbili ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo, Baba wa Taifa Hayati, Mwl. J.K. Nyerere wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong wa China.

Msisitizo huwa umetolewa wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo alipokutana na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Prof. Hao Ping na ujumbe wake katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Aidha, katika mazungumzo hayo Mhe. Londo ameueleza ujumbe huo kuwa Tanzania ina thamani ushirikiano imara uliopo kati yake na China hasa wakati huu ambapo mataifa hayo yanaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia tangu kuanzishhwa kwake.

Pia, ameipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kuandaa na kuwa mwenyeji wa Mkutano wa kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba, 2024 jijini Beijing, China.

Alisema kuwa kupitia mkutano huo Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye matokeo makubwa kiuchumi zilisainiwa ikiwemo ya kufufua reli ya TAZARA ambayo ilijengwa enzi za uhuru wa Tanganyika.

‘’ Maboresho ya Reli ya TAZARA inayoiunganisha Tanzania na Zambia ni hatua muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi hizo mbili pamoja na ukanda wa kusini mwa Afrika ambao unategemea bandari ya Dar Es Salaam katika usafirishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali’’ alisema Mhe. Londo.

Pia, alieleza mradi huo ni alama kubwa na ya kwanza ya miradi ya ushirikiano kati ya Tanzania na China iliyoacha kumbukumbu isiyofutika kwa pande zote mbili na kwamba historia hiyo imeendelea kurithishwa kwa kizazi cha sasa kupitia manufaa yake katika shughuli za kiuchumi.

Kadhalika, ameeleza imani yake juu ya ziara ya Kamati hiyo na kwamba itaenda kufungua ushirikiano zaidi wa kibunge kati ya Bunge la Tanzania na Bunge la China.

Vilevile ameshukuru kwa ufadhili wa fursa za masomo ya muda mrefu na mfupi ambao umekuwa ukitolewa na Serikali ya China kwa Tanzania na hivyo kuendelea kukuza ushirikiano miongoni wa wananchi wa mataifa hayo.

Kwa upande wa Prof. Ping ameeleza kuwa jitihada zinazofanywa sasa na viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping zinaonesha nia ya dhati ya kukuza ushirikiano huo wa kihistoria.

‘’Ushirikiano katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa utaendelea kuimarishwa na kudumishwa na tuhakikisha yale yote yaliyokubaliwa na viongozi wetu wakuu wakati wa mkutano wa FOCAC yanasimamiwa na kutekelezwa kwa maslahi ya pande zote mbili’’ alisema Prof. Ping.

Pia ameeleza kuwa Mkutano wa 20 wa Chama cha Kikomunist cha China ulifanya mageuzi katika maeneo ya kimkakati ya ushirikiano baina ya Tanzania na China na Afrika kwa ujumla ambayo yameongeza mafanikio katika urafiki wa mataifa hayo na kuruhusu utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kisekta.

Pamoja na masuala hayo viongozi hao pia wameahidi kuendelea kushirikiana kwa kuunga mkono sera za kitaifa na ajenda mbalimbali katika majukwa ya kikanda na kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa wananchi wa mataifa hayo mawili ili kukuza mawasiliano yatakayorahisisha kukuza sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya siku 3 ambapo unatarajia kukutana na kuzungumza na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb.)

 

Related Posts