Tanzania Prisons kimkakati zaidi | Mwanaspoti

HESABU walizonazo Tanzania Prisons ni kuhakikisha kwamba, hawataki kuwaruhusu wapinzani wao, JKT Tanzania kupata hata pointi moja watakapokutana wikiendi hii.

Prisons wanaamini kwamba, kitendo cha kuwapa mwanya JKT Tanzania kupata pointi moja, kitawaharibia zaidi kutokana na hivi sasa msimamo wa ligi ulivyo.

Timu hizo zinakutana Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar huku zote zikiwa na pointi 10, JKT Tanzania ikishika nafasi ya 11 wakati Prisons ni ya 12.

JKT Tanzania ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo, wamecheza mechi tisa, wakati wenzao Prisons wakishuka dimbani mara 10.

Kupishana mchezo mmoja huku zote zikiwa na pointi kumi, kumemfanya Kocha wa Prisons, Mbwana Makata kuiandaa timu yake kimkakati zaidi ili kufanikisha lengo lao la kupata ushindi.

“Sisi tuna pointi kumi na wao wana kumi, hivyo yeyote atakayefungwa atamshusha mwenzake.

“Kutokana na hali hiyo, ni wazi mchezo huo ni muhimu sana kwetu kushinda japo tunaamini haitokuwa rahisi,” alisema Makata na kuongeza.

“Wakati ligi imesimama, tulikuwa na program ya gym angalau mara mbili kwa wiki ili kulinda utimamu wa mwili kwa wachezaji, hiyo itasaidia kutufanya tuwe fiti hadi kufikia siku ya mchezo.”

Takwimu zinaonyesha kuwa, tangu mwaka 2018, JKT Tanzania imepata ushindi mmoja pekee katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons. Kwa upande mwingine, Prisons imeibuka kidedea mara nne, huku mechi tano zikimalizika kwa sare.

Hata hivyo, katika mechi tatu zilizopita, timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1 mfululizo.

Related Posts