Songwe. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe kwa mahojiano baada ya kile kinachoelezwa kukiuka utaratibu wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 22 Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga amethibitisha kumshikilia kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini pamoja na watu wengine.
“Ni kweli tunaashikilia Mbowe na viongozi wengine japo idadi yao bado sijaipata, kwa mahojiano zaidi kutokana na kukiuka utaratibu wa kampeni.
“Aliposhuka uwanja wa ndege alipopokelewa kusalimia akataka kuweka na mkutano hapohapo, jambo ambalo si sahihi kwa kuwa vyama vyote viliwasilisha maeneo ya mikutano yao,” amesema kamanda huyo.
Ametoa rai kwa vyama vyote kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi akieleza kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayeenda kinyume, hasa kipindi hiki.
Kauli hiyo imetolewa baada ya taarifa kusambaa kwenye mitando ya kijamii, ikizungumzia tukio la kukamatwa kwa Mbowe.
Mkurugenzi wa mambo ya Nje na Mawasiliano wa Chadema, John Mrema ameandika kwenye ukurasa wake wa X: “Jeshi la Polisi limevamia msafara wa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mheshimiwa Freeman Mbowe akiwa njiani kuelekea Vwawa, Wilaya ya Mbozi kwenye uzinduzi wa kampeni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mchana huu.”
Baadaye taarifa iliyotolewa na Chadema imelaani hatua hiyo ya polisi kumkamata Mbowe na viongozi mbalimbali alioambatana nao.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, Mrema, imesema msafara wa Mbowe ulikuwa umeshafanya mikutano ya kampeni katika Kata ya Itaka, Kijiji Cha Itewe na Kata ya Halungu Mjini.
“Awali mkutano wa kwanza uliokuwa ufanyike katika mji wa Mlowo uliozuiliwa na polisi pamoja na wenyeji wetu ambao ni Chama Cha ACT Wazalendo kutualika kushiriki kwenye mkutano wa pamoja, ila Polisi walikataa na kutawanya wananchi kwa mabomu ya machozi,” imeandika taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo Chadema imewataja waliokamatwa mbali na Mbowe kuwa ni, Joseph Mbilinyi (Mwenyekiti Kanda ya Nyassa), Pascal Haonga (Mbunge wa zamani Mbozi Mashariki), Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Wilaya ya Mbozi (hakutajwa jina) na Appolinary Boniface (mkuu wa Digital Platform).
Wengine ni Paul Joseph (ofisa habari Kanda ya Nyassa), Calvin Ndabila (ofisa habari Kanda ya Nyassa), Mdude Nyagali (Mwanaharakati na kada wa Chadema) na wasaidizi wa Mbowe (Bwire, Adamoo na Lingwenya).
“Polisi wameondoka na viongozi wetu na hawajasema wanawapeleka wapi na mpaka sasa hatujui wanashikiliwa wapi na kwa sababu gani,” imeandika taarifa hiyo.
Mrema katika taarifa hiyo amelitaka Jeshi la Polisi liwaachie mara moja na bila masharti yoyote ili waendelee na ratiba ya kampeni na ameialika jumuiya ya kimataifa kuja kushuhudia alichokiitka uvunjifu wa haki za kidemokrasia.