Wahitimu fani ya ufundi mitambo wapewa mbinu za ajira

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Wahitimu wa fani ya ufundi na uendeshaji mitambo mikubwa kutoka Chuo cha IHET, wametakiwa kuchangamkia fursa ya soko la ajira lililopo nchini kutokana na uhitaji mkubwa wa watu wenye utaalamu huo nchini katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, DCP Ramadhani Ng’anzi wakati wa mahafali ya nne ya Chuo cha Mitambo na Teknolojia cha IHET yaliyofanyika leo Novemba 22, 2024 kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaaam.

DCP Ng’anzi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amesema wahitimu hao tayari soko linawasubiri, kwani wana fursa ya kufanya kazi katika maeneo mengi kama vile madini, nishati, ujenzi na kilimo.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, DCP Ramadhani Ng’anzi, akimkabidhi tuzo Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Teknolojia na Mitambo, Mohamed Mpinga wakati wa mahafali ya 4 ya Chuo hicho jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa soko bado ni kutokana na wanaohitimu mafunzo hayo kuwa wachache nchini, hivyo ni jukumu la kila mhitimu kujipanga kuhakikisha ananufaika na fursa zilizopo kupitia fani ya uendeshaji mitambo mikubwa na teknolojia.

“Soko la ajira kama lilivyo linawasubiri. Mahitaji na matumizi ya mitambo mikubwa yameongezeka kutokana na utekelezaji wa miradi inayondelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini na shughuli za kiuchumi,” amesema DCP Ng’anzi.

Amefafanua kuwa ununuzi wa mitambo ni gharama kubwa, inahitaji watu wenye weledi na utaalamu katika kuitumia, hivyo kuwataka wahitimu hao kwenda kutafuta suluhisho la matatizo yaliyopo endapo watapata nafasi ya kufanya kazi katika maeneo hayo.

Aidha amewasisitiza kujitolea ili kupata uzoefu wakujifunza zaidi kivitendo na wasiridhike na elimu waliyoipata chuoni hapo bali kujiendeleza zaidi kwanj teknolojia inabadilika kila mara.

Naye Mkuu wa Chuo cha IHET, Asia Ntembo amesema chuo hicho kimenzishwa mwaka 2017 kikiwa na usajili wa kudumu na kimefanikiwa kupokea wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi.

“Chuo cha Mitambo IHET kimejikita katika kutoa kozi za muda mrefu na mfupi katika fani za ufundi wa mitambo, umeme wa magari, ufundi wa magari, tehama na opereta wa mitambo.

“Malengo ya chuo ni kufikisha wahitimu 2000 kufikia mwaka 2026 kwani tangu kimeanziashwa wahitimu jumla ni 1701 “, ameeleza mkuu wa chuo hicho.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo, DCP Mstaafu, Mohammed Mpinga, amezishukuru taasisi mbalimbali za Serikali kutoa ushauri kuhakikisha wanajenga msingi mzuri wa matumizi ya mitambo.

Amesema malengo yao ni kutengeneza wataalamu na kuondoa utegemezi wa wataalamu wa mitambo kutoka nje ya nchi na katika kuuunga mkono juhudi za Serikali Chuo kimetoa ufadhiri wa wanafunzi 20 kupitia program ya Mwanagenzi.

“Jukumu la Bodi ni kusimamia na kushauri chuo ili kutimiza malengo, kuhamasisha maendeleo ya chuo na kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi kwa kuzingatia dira na malengo ya kuanzishwa kwa chuo,” amesema Mpinga.

Related Posts