Na Muhidin Mmanja,Kilwa
WAKAZI wa kijiji cha Kiranjeranje wilaya ya Kilwa mkoani Lindi,wameiomba Serikali kuwajengea kituo cha afya ili waondokane na adha ya kutembea kilometa zaidi ya 70 kwenda kupata huduma za matibabu Hospitali ya mkoa Lindi(Sokoine).
Kijiji cha Kiranjeranje kina wakazi zaidi ya 5,000 kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambao kwa sasa wanategemea kupata huduma za matibabu kwenye zahanati ndogo ambayo haikidhi mahitaji kutokana na ongezeko kubwa la watu waliopo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema,ni muhimu kwa Serikali kujenga kituo kituo cha afya badala ya kutegemea zahanati ambayo haina huduma muhimu kama vile upasuaji mkubwa,huduma za x-ray,jengo la mama na mtoto na wodi ya kulaza wagonjwa.
Mkazi wa kijiji hicho Juma Kingwande alisema,kutokana na kukosekana kwa huduma hizo wanalazimika kutumia gharama kubwa kati ya Sh.5,000 hadi 7,000 kwa ajili ya nauli ya kwenda Lindi mjini wanapohitaji kupata huduma muhimu zaidi ya uchunguzi.
Kingwande alieleza kuwa,kijiji cha Kiranjeranje kina ongezeko kubwa la watu wanaofika kwa ajili ya kuanzisha makazi ya kudumu,kufanya biashara wakiwemo jamii ya wafuagaji wanaofika kwa wingi kwa ajili ya shughuli zao.
“tunaiomba Serikali ya awamu ya sita chini ya Mama yetu Dkt Samia Suluhu Hassan,ituangalie kwa jicho la huruma ili tuondokane na changamoto ya kusafiri umbali mrefu na kutumia muda mwingi kwenda kufuata huduma za matibabu katika Hospitali ya Sokoine Lindi mjini”alisema Kingwande.
Aidha Kingwande,ameiomba Wizara ya ujenzi kutekeleza ahadi ya kujenga barabara ya Kiranjeranje-Nanjilinji hadi Ruangwa kwa kiwango cha lami ambayo imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Alisema,barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kiuchumi kwani ndiyo inayotumika kusafirisha mazao mbalimbali kama ufuta,korosho,mbaazi na mazao mengine yanayozalishwa kwenye vijiji vinavyopitiwa na barabara hiyo.
Kwa mujibu wa Kingwande,barabara hiyo itakapojengwa kwa lami itasaidia kuunganisha wilaya ya kilwa na wilaya nyingine za mkoa wa Lindi na mkoa jirani wa Ruvuma.
Mkazi mwingine Seleman Ndope alisema,kutokana na wingi wa watu kuna kila sababu kwa Serikali kuboresha huduma za matibabu kwa kujenga kituo cha afya badala ya kutegemea zahanati ya kijiji ambayo imeelemewa na wagonjwa wengi wanaofika kufuata huduma za afya.
Ndope,ameikumbusha Serikali kutekeleza mpango wake wa kujenga vituo vya afya kwa kila kata hapa nchini na ahadi ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa aliyotoa mwaka 2020 kuwa,serikali itajenga kituo cha afya Kiranjeranje ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya ambazo hazitolewi kwenye ngazi ya zahanati.
Ndope alisema,kijiji hicho kina mchango mkubwa kwa uchumi wa wilaya ya Kilwa na mkoa wa Lindi kwa ujumla kutokana na kubarikiwa kuwa na madini mengi ya Jipsam,sementi na wakazi wake ni wakulima wakubwa wa ufuta unaochangia mapato ya Halmashauri ya wilaya Kilwa.
Alieleza kuwa,baadhi ya watu hasa mama wajawazito wanapoteza maisha wakiwa njiani wanapokwenda Lindi mjini kufuata huduma ya kujifungua hasa wale wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa ambapo huduma hizo hazipatikana kwenye zahanati ya kijiji chao.
“kwa sasa kijiji chetu kina watu wengi hasa wageni wanaokuja kila siku kufanya shughuli mbalimbali,changamoto kubwa ni ukosefu wa huduma bora za afya,tuna zahanati ndogo yenye wahudumu wachache,lakini baadhi ya huduma hazipatikani na tunatumia gharama kubwa na muda mwingi kwenda Lindi kufuata matibabu”alisema Ndope.
Alieleza kuwa,kutokana na mahitaji ya kituo cha afya,serikali ya kijiji na wananchi imetenga ekari zaidi ya 5 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya miaka mitatu iliyopita,lakini tangu wakati huo eneo hilo halijaendelezwa na wananchi wanaendelea kuteseka.
Fadhil Kitengu alisema,iwapo Serikali itajenga kituo cha afya na kuimarisha miundombinu ya barabara zitakazounganisha kijiji hicho na wilaya nyingine za mkoa wa Lindi mapato ya Halmashauri yataongezeka kwa sababu wananchi hawatapoteza muda wao kwenda nje ya kijiji hicho kufuata huduma za afya.
Hamis Msigala,ameiomba Serikali kupitia wizara ya afya kuharakikisha mchakato wa ujenzi wa kituo cha afya ili waweze kupata huduma za matibabu karibu ili kuwaondolea usumbufu kwenda hadi Kitomanga au Hospitali ya mkoa Sokoine kufuata matatibu.
“Kijiji cha Kiranjeranje kina sifa ya kupata kituo cha afya kutokana na idadi ya watu wake na ndiyo makao makuu ya kata ya Kiranjeranje yenye wakazi takribani 16,375 ipo haja kwa Serikali kutujengea kituo cha afya ili tuweze kupata baadhi ya huduma kama za upasuaji na kulaza wagonjwa ambazo kwa sasa hazipatikani”alisema.
Baadhi ya nyumba bora na za kisasa
zinazoendelea kujengwa katika kijiji cha Kiranjeranje wilaya ya Kilwa
mkoani Lindi,wakazi wa kijiji hicho wanaiomba Serikali kuwajengea kituo
cha afya ili waweze kupata huduma bora za matibabu badala ya kutegemea
zahanati ndogo ambayo baadhi ya huduma zikiwemo za upasuaji na kulaza
wagonjwa hazipatikani