Sikonge, Tabora.Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia watu nne kwa tuhuma za kuuza mifuko 600 ya mbolea aina ya NPK 101824 inayotumika kupandia tumbaku. Mbolea hiyo, yenye thamani ya Sh88 milioni, ni mali ya kampuni ya Mkwawa Tobaco Limited.
Akizungumza leo, Novemba 22, 2024, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 24, 2024, katika Wilaya ya Sikonge.
Kwa mujibu wa Kamanda Abwao, Michael Mashaka, meneja wa kampuni ya Mkwawa Tobaco Limited, aligundua kuibiwa kwa mbolea hiyo na uchunguzi ulionyesha kwamba gari lililokuwa limebeba mbolea hiyo, halikufikisha mzigo ilikotakiwa.
Badala yake, mzigo ulishushwa mkoani Katavi na kuuzwa kwa mfanyabiashara wa pembejeo, Cross William Sanagala kwa Sh20 milioni badala ya thamani yake ya Sh88 milioni.
Kamanda Abwao amesema mfanyabiashara huyo alikimbia baada ya kununua mbolea hiyo na juhudi za kumtafuta zinaendelea. Polisi wanamtaka ajisalimishe kituo chochote kwa usalama wake.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Paul Biria (49), Tito Haule (48), Athuman Kilatu (33) na Eneza Nyika (37), ofisa wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Katavi.
Kamanda Abwao ameongeza kuwa mifuko yote 600 ya mbolea hiyo imepatikana na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema mbolea hiyo ingeweza kupandia tumbaku katika ekari 150.
“Kukamatwa kwa mbolea hii kumeokoa wakulima wa tumbaku kupata hasara kubwa msimu huu wa kilimo,” amesema Chacha.
Pia, ametoa motisha kwa maafisa wa polisi waliofanikisha kurejesha mbolea hiyo.