Wenye malori nao wautaka mradi wa mwendokasi

Dar es Salaam. Chama cha Wamiliki wa malori wa Kati na Wadogo (Tamstoa), kimeonyesha nia yake ya kutaka kuwekeza katika mradi wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi, huku kikiomba kufupishwa kwa michakato katika kuingia ubia huo.

Tamstoa imeonyesha nia hiyo leo Ijumaa Novemba 22, 2024 walipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia Tanzania, David Kafulila, ambapo pamoja na mambo mengine walitaka kujua taratibu za kufuata ili kufanikisha hilo.

Wafanyabishara hao wanakuja na ombi hilo, wakati kukiwa na malalamiko ya uchache wa mabasi hayo, jambo linalowafanya abiria kusubiri kwa muda mrefu vituoni.

Mradi huo ulioanza mwaka 2016 katika awamu ya kwanza ulihusisha barabara ya Morogoro, ulianza na mabasi 140 na baadaye yakaongezwa mabasi 70, lakini hadi kufika mwaka jana kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalaam, Albert Chalamila,  mabasi zaidi ya 70 yalikuwa yameharibika na kutofanya kazi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa chama hicho, Chuki Shabani, amesema wawekezaji wazawa wameona wanao uwezo wa kuendesha mradi huo ili kuwaondolea adha ya usafiri huo Watanzania.

“Kutokana na nia hiyo tumeamua kutafuta muda wa kukutana na mkurugenzi aweze kutupa elimu tunafanyaje ili hilo liweze kufanyika kwani tupo tayari kuwekeza kwenye mradi huo hata kesho,”amesema Shabani.

Pamoja na nia hiyo, ameomba kurahisishwa mchakato wa kuweza na kueleza kuwa  wawekezaji wengi  katika sekta hiyo,  hawana uelewa na michakato zaidi ya kuhisi wanacheleweshwa.

 “Wengi wetu ni wawekezaji hapa, lakini hatuna elimu ya hivyo ya darasani, tunachotoka kutoka kwa Serikali ni kutuambia barabara hii mnaweza kuleta mabasi kadhaa kwa kuwa fedha tunazo na zingine zipo kwenye benki, hatutaki kuelezwa mambo ya michakato ipo sijui katika hatua gani,”amesema.

Akieleza nini watafanya endapo watafanikiwa, mwenyekiti huyo amesema wana imani kutoa huduma bora kwa kuwa wao ni wafanyabiashara.

Kwa upande wake, Kafulila, amewaondoa hofu wafanyabiashara hao kuhusu michakato katika kuwekeza katika mradi huo, kwa kile alichoeleza yamefanyika marekebisho ya sheria katika masuala ya ubia.

“ Ni kweli kulikuwa na ugumu fulani wa sheria, lakini baada ya kurekebishwa kwa sheria za ubia na kanuni zake mwaka jana(2023), mwitikio kwa wawekezaji umekuwa mkubwa na Watanzania wategemee michakato ya kuwekeza kwa ubia itachukua muda mfupi hata miezi miwili,”amesema.

 Amefafanua kuwa utekelezaji wa miradi ya PPP ulianza wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, ambapo mwaka 2009 ilitungwa sera ya PPP na mwaka 2010 ilitungwa sheria na kufuatiwa na kanuni zilizotungwa mwaka 2011.

“ Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2014 na kufuatia marekebisho mengine ya sheria hiyo yaliofanyika mwaka 2018”, amesema Kafulila.

Kuhusu wazawa kupewa kipaumbele, amesema hilo ni kipaumbelea kuanzia kwenye sheria za nchi, sera lakini kubwa ni msimamo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wazwa wanapewa fursa zaidi.

“Kwa hiyo mimi nimewaambia wao wakakae wakabainishe waone ni nani na nani ambao wako tayari kwa ajili ya kufanya mradi huu wa mabasi,” amesema Kafulila.

 Amesema hadi sasa mradi huo una awamu sita na awamu ya kwanza na ya pili ndio zimepiga hatua katika utaratibu za kumpata mbia.

Kafulila amebainisha kuwa kuna awamu nne ambazo ziko wazi na sheria imeruhusu wawekezaji wenyewe kuja na mapendekezo.

Kuhusu mradi wa mwendokasi awamu ya pili amesema tayari wawekezaji 14 wameonyesha nia ya kutaka kuuendesha huku ule wa kwanza aliyejitokeza ni mmoja.

Akitoa maoni yake kuhusu maamuzi hayo ya Tamstoa, Mhadhiri Mwandamizi katika masuala ya uchumi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya, Dk Balozi Morwa, amesema ni jambo zuri kwa kuwa wao wanaijua sekta ya usafirishaji vilivyo kuliko hata watendaji wa Serikali waliopo kwenye mradi huo.

Dk Morwa amesema Serikali itaweza kupata kodi kwani sasa hivi katika mradi huo inaendeshwa kwa kupitia kodi za wananchi.

“Vilevile itachochea uchumi kwa watu kufika maeneo yao ya kazi mapema kwa kuwa awamu ya kwanza ambapo usafiri huo umeanza saa za kufika maeneo ya uzalishaji zimepungua licha ya kuwepo kwa changamoto za uhaba wa mabasi hayo,”amesema.

Dart watoa ofa ya kadi janja

Katika hatua nyingine, Wakala wa usafiri wa mabasi yaendayo Haraka(Dart), umetoa ofa katika ununuaji wa kadi janja kuelekea msimu  wa sikukuu ambapo kwa sasa abiria akinunua kadi hiyo atapata ofa ya safari nne tofauti na awali ambapo ilipaswa aweke tena hela kwa ajili ya nauli.

Akitangaza maamuzi hayo jana, Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia, amesema wamefanya hivyo kwa lengo la kuwamasisha wananchi kuhamia katika kadi.

“Tunafanya hivyo ili kuwahamasisha abiria kuachana na mfumo wa tiketi ambao mbali na kuwaondolea usumbufu wa kupanga foleni, lakini pia zinasaidia Serikali kudhibiti mapato yake moja kwa moja,”amesema Dk Kihamia.

Related Posts