KOCHA mpya wa Yanga, Sead Ramovic jana jioni alitarajiwa kuwa na kikosi chake kamili baada ya mastaa wa timu hiyo waliokuwa wanayawakilisha mataifa yao kurejea lakini huko mambo yameanza kuiva taratibu.
Kwenye mazoezi ya siku tatu chini ya kocha huyo tangu aanze kazi, kuna mambo matatu ameanza nayo ambayo yanaonyesha kuwa baada ya muda mfupi kuna mambo yatabadilika.
Kocha huyo amekuwa akitumia saa mbili kila siku jioni kukiandaa kikosi cha timu hiyo, kwanza ameshusha mkwara mzito kwamba maisha ndani ya kikosi hicho yanaanza upya na kila mchezaji ataanza kujitafutia nafasi upya na lazima awe na juhudi na mazoezi ili aweze kupata nafasi.
Hata hivyo, siku ya kwanza aliwashtua zaidi baada ya kuwaambia wachezaji wake kama kwenye kundi lao kuna staa hamfahamu basi hawatazidi wawili na kwamba wengine wote anawafahamu tena huku akiwataja kwa majina hatua iliyowashtua wachezaji wa timu hiyo.
Kwenye kikao chake cha kwanza na wachezaji hao, Ramovic amewajaza upepo akiwaambia timu hiyo ina wachezaji wenye vipaji vikubwa ambavyo lazima wavitumie kwa nguvu ili kuzizidi timu nyingine kisha wachukue ubingwa na hilo hatakuwa na masikhara nalo.
Akiwa kwenye uwanja wa mazoezi pale Avic Town Kigamboni, Ramovic ameanza kuingiza vitu fulani hivi ambavyo havitofautiani sana na vile vya mtangulizi wake Miguel Gamondi akitaka sana soka la kasi kuelekea lango la wapinzani na mabao yafungwe.
Kama unataka kumtibua kocha huyo basi tembea uwanjani, ambapo amekuwa akitaka kuona kila mchezaji anakuwa mchezoni kutengeneza nafasi na kuongeza idadi wakati wanashambulia na hata wakati wamepoteza mpira.
Ramovic ambaye anasaidiwa na Mustafa Kodro, muda wote wako mchezoni wakifuatilia kila hatua na mazoezini ukipatia tu wanatoa mzuka kwa wachezaji wao kwa kuwapongeza kwa makofi ili kuongeza nafasi ya mchezaji kujiamini, lakini mara kwa mara wamekuwa na vikao vifupi mazoezini wakijadili baadhi ya mambo.
Mmoja wa mastaa wa timu hiyo ameliambia Mwanaspoti kwamba kocha huyo amewatangazia haraka kwamba hana masihara na mchezaji wake atakayeonyesha kukosa nidhamu.
“Hapo kwenye nidhamu nadhani kila mmoja wetu anatakiwa kuwa makini, kocha (Ramovic) hataki kuona kabisa mambo ya kukosa nidhamu ametuambia mapema kwamba kama kuna mtu hawezi basi ajiweke kando na anataka kambi iheshimiwe na kila mmoja,” alisema staa huyo anayecheza nafasi ya beki.
“Ni kocha mzuri sana nilivyomuona kwa siku mbili hizi, kitu muhimu kwake anataka watu kujituma, kila mtu aonyeshe anataka nafasi na atampa, kitu alichotushtua ni pale aliposema kila mtu anamfahamu kwenye timu yetu tena anatutaja kwa majina.
“Hii inaonyesha kwamba alikuwa anatufuatilia au alipata muda wa kutosha kuijua timu, kifupi ni kocha mzuri, anaelekeza kwa utaratibu na kufanya kwa vitendo ngoja tukamilike halafu tutaona zaidi mambo yake.”
Mkwara huo wa Ramovic ukaamsha ushindani mpya ndani ya timu hiyo kwa kila mchezaji kuanza kuonyesha anaitaka nafasi ambapo kila staa amekuwa zaidi ya siriazi akijitafutia ufalme mpya chini ya kocha huyo.
“Unajua hatumsemi vibaya kocha aliyepita lakini kuna wakati alikuwa anakatisha tamaa unajituma lakini bado unaona nafasi ni ngumu kupata lakini ukifika mazoezini sasa utaona mambo yalivyobadilika,” alisema staa mwingine anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
“Unajua ametuambia wazi kwamba kama ukimuonyesha juhudi mazoezini kwenye mechi atakupa nafasi, hatapanga timu kutokana na jina la mtu, hii itasaidia maana sasa mambo yatabadilika.”
Hali hiyo inatoa matumaini mapya kwa wachezaji ambao hawakuwa na wakati mzuri kipindi cha Gamondi akiwamo Kibwana Shomari na Aboutwalib Mshery ambao hawakucheza mechi yoyote msimu huu kama ilivyokuwa kwa Farid Mussa aliyepona hivi karibuni.
Mbali hao, pia Khomeiny Abubakary, Nickson Kibabage, Aziz Andabwile, Jonas Mkude, Salum Abubakar, Shekhan Khamis, Denis Nkane, Jean Baleke na Kennedy Musonda ambao ishu ya kupata nafasi kipindi cha Gamondi ilikuwa sio uhakika lakini sasa wanaweza kubadili upepo.