Zanzibar ilivyojizatiti kuondoa urasimu bandarini

Unguja. Ukizinduliwa mpango wa maboresho ya huduma za bandari, Rais wa Zanzibar , Dk Hussein Mwinyi amesema utaleta mageuzi ya kiutendaji na kuondoa urasimu kwa kupeana majukumu kwa kila anayehusika kupitia viashiria vilivyowekwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliondaliwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kushirikiana na Taasisi ya Tony Blair (TBI) leo Novemba 22, 2024 Ikulu Zanzibar, Rais Mwinyi amezitaka taasisi hizo kuwa tayari kuutekeleza ili ulete tija.

Mpango huo pia unazihusisha wizara tatu za Ujenzi, Biashara na Fedha na taasisi 16.

Dk Mwinyi amesema: “Iwapo kuna mmoja katika mnyororo huo hatimizi wajibu wake, atafanya kazi nzima isiende inavyotakiwa, na itabidi wafanye tathimini kila wakati kupitia viashiria vilivyowekwa na wale ambao watashindwa kutekeleza hilo nitapenda kupata taarifa ili tuchukue hatua stahiki.”

“Endapo taasisi zote zitafanya kama inavyotakiwa hakika tutapata mafanikio makubwa katika nchi yetu, hivi sasa nchi kama za Singapore, Gambia na Kenya wanatumia mfumo huo wa ushirikishwaji na wameweza kupata mafanikio makubwa,” amesema Dk Mwinyi.

Ametaja malengo mengine ya mpango huo ni kurahisiha ushushaji wa makasha, kupunguza muda wa meli kukaa ukutani na kupunguza muda wa meli kukaa nangani, hivyo kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini na kuongeza ukuaji wa uchumi.

Dk Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kuendesha huduma za bandari kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia bandari ni mlango mkuu wa uchumi wa nchi.

Amesema mikakati ya Serikali ya ukuzaji uchumi Zanzibar inaendelea kuwawekea wafanyabiashara mazingira mazuri na sasa inatarajia kuanza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuendeleza sekta ya bandari nchini na miongoni mwa mipango ni kuimarisha bandari za Malindi, Shumba, Mkoani, Pemba,” amesema.

Amewataa wadau wote zikiwemo kampuni za uendeshaji wa bandari, mamlaka za forodha, mamlaka za udhibiti wa bidhaa zinazoingia bandarini, kampuni za utoaji wa mizigo na mamlaka zinazohusika na ulinzi na usalama bandarini kuwa tayari kutekeleza mpango huu kwa vitendo kufikia malengo yake.

“Unapokuwa na ufanisi wa bandari ambayo ndiyo mlango mkuu wa uchumi bila shaka athari zake zinakuwa kubwa zaidi, kwa hiyo tusiishie kutia saini tuhakikishe tunayatekeleza haya,” amesema.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Mohamed Salim amesema Bandari ya Malindi ni ndogo, ilijengwa mwaka 1920 na wakati huo idadi ya wananchi walikuwa wacheche na mahitaji yalikuwa madogo lakini kwa sasa kila kitu kinaongezeka.

Dk Khalid amesema kipindi cha nyuma kumekuwapo msongamano mkubwa, vifaa vicheche, taaluma ndogo na malalamiko mengi, meli zilikuwa zikichelewa zikikaa nangani kwa zaidi ya siku 32 katika Bandari ya Malindi.

“Kutokana na hali hiyo, wapo baadhi ya watu waliamua kutoleta meli zao Zanzibar na kuzipeleka Mombasa, Kenya nyingine kwenda Dar es Salaam, huku bei ya kuleta makontena Zanzibar ilikuwa kubwa hivyo hali ya maisha ilipanda sana,” amesema.

Amesema baada ya Serikali kuanza kuchukua hatua za kufanya maboresho ya bandari hiyo na kumpa mwendeshaji kampuni ya kigeni kutoka Ufaransa ya AGL, kupitia kampuni tanzu ya Zanzibar Multpurpose Terminal (ZMT) takribani Dola 80 milioni za Marekani (Sh212 bilioni) zimeokolewa.

Amesema fedha hizo zilikuwa zinatumika nje ya Zanzibar kuhudumia usafiri wa makontena na kukaa meli muda mrefu katika Bandari ya Malindi.

“Lakini katika kuongeza ufanisi wa bandari, Rais aliagiza kushirikiana na Taasisi ya Tony Blair kuandaa mpango wa maboresho wa huduma za bandari ambao umeshirikisha wadau wote, zikiwemo kampuni za meli za kigeni za wazawa na watu wa forodha,” amesema.

Amesema mpango huo umeshirikisha watu wote na wameweka viashiria vya utekelezaji mzuri ambao utakuwa na maeneo ya maboresho katika huduma za bandari kwa upande wa baharini na huduma za bandari baada ya meli kufika nangani na kupata ukuta isikae zaidi ya siku tatu, huku ushushaji na upandishaji wa makontena kwa meli kubwa mzunguko wake uwe chini.

Katika kuleta ufanisi zaidi, Dk Khalid amesema wataunda kamati itakayowashirikisha wadau wote watakuwa wakikutana kila baada ya miezi mitatu, miezi sita na mwaka mmoja ambao unakuwa wa kuangalia ufanisi wa jumla.

Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Akif Ali Khamis amesema wataboresha maeneo makubwa manne ambayo ni kuona namna gani ukuta unatumika katika utoaji wa huduma na namna ya kuboresha ufanisi katika kutoa huduma ndani ya saa moja, hivyo kupunguza gharama kwa kadri meli inavyokaa nangani.

Katibu Mkuu wa Mawakala wa Forodha Zanzibar, Ahmed Nassor amesema mpango huo utaondoa changamoto zilizokuwa zinaikumba bandari hiyo.

“Mategemeo yetu ikiwa watashirikishwa wadau wote italeta mafaniko makubwa katika bandari hasa katika eneo la ufungaji na ushushaji wa mizigo, sisi tumeona kutoka makontena saba kwa saa hadi kufika makontena 17 kwa sasa, si kazi ndogo,” amesema.

Related Posts