Zigo kwa kamati ya uchunguzi Kariakoo

Dar es Salaam. Wakati kamati ya uchunguzi wa ajali ya jengo lililoporomoka Kariakoo na masuala mengineyo ikianza kazi, wataalamu na wenyeji wa eneo hilo, wamebainisha madudu lukuki ambayo kamati hiyo haiwezi kuepuka kukutana nayo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeingia kazini jana Novemba 21, 2024 kufanya uchunguzi kutokana na kuporomoka jengo la ghorofa nne lililopo mtaa wa Mchikichi na Congo.

Jengo hilo lililoporomoka Novemba 16, saa tatu asubuhi lilisababisha vifo vya watu 20 huku wengine 88 wakiokolewa. Shughuli ya uokoaji imefanyika kwa siku nne na sasa kazi inayoendelea ni kuondoa mizigo na kulibomoa jengo hilo.

Kamati ya wataalamu iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, itachunguza jengo hilo lililoporomoka, majengo mengine yanayoendelea kutumika katika eneo la Kariakoo na uimara wa majengo yanayojengwa.

Majaliwa alisema pia itachunguza endapo taratibu zinazingatiwa wakati wa ujenzi ikiwemo vibali, makandarasi wenye sifa na usimamizi wa mamlaka husika wakati wa ujenzi.

Alisema kamati hiyo imeundwa ichunguze endapo uboreshaji wa majengo unaofanywa Kariakoo unazingatia sheria, kanuni na taratibu na kubainisha majengo yote yaliyo katika hatari ya kuanguka na kupendekeza hatua za kuchukua.

Wakati kamati ikiingia kazini, ni dhahiri inakwenda kukutana na madudu lukuki kutokana na uwepo wa ripoti za awali zilizotolewa na kamati zingine zilizoundwa baada ya majengo mengine kuporomoka.

Miongoni mwa ripoti hizo ni ya kamati iliyoundwa mwaka 2006 na aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Lowassa.

Kamati hiyo ilibaini majengo 147 kati ya 505 yaliyokaguliwa jijini Dar es Salaam hayakuwa na nyaraka na vibali sahihi vya ujenzi.

Mwaka 2008, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyempokea kijiti Lowassa aliliambia Bunge kwamba kamati  iligundua kuwa kanuni zilikiukwa kwenye ujenzi wa nyumba 81 na wamiliki wa majengo 22 hawakufahamika.

Si hivyo tu, Machi 29, 2013 jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi lilianguka na kusababisha vifo vya watu 36, sababu ya kuporomoka ikitajwa kuwa ujenzi usiozingatia utaalamu.

Kutokana na hilo, Novemba 5, 2013, kampuni ya Design Plus Architects (DPA) iliyopewa zabuni ya kukagua majengo Manispaa ya Ilala, ambayo Kariakoo imo, ilibaini kati ya majengo ya ghorofa 90 yaliyokaguliwa, 67 yalikuwa yamejengwa kinyume cha sheria.

Kampuni hiyo ilisema baadhi ya majengo hayo yanaweza kuporomoka kutokana na ujenzi wake kuwa chini ya kiwango. Ukaguzi ulianza Julai 2013 baada ya zabuni kutolewa.

Jumatano, Novemba 20, Rais Samia alipofika kujionea hali halisi ya jengo lililoporomoka na kuzungumza na wafanyabiashara na wananchi, alisema Serikali haitasita kubomoa majengo yote ya Kariakoo iwapo kamati iliyoundwa kuchunguza usalama wake, itashauri ifanyike hivyo.

“Sasa tume imeona nini, imesema nini, imetushauri nini, kama tume itatushauri tuendelee kubomoa majengo yasiyokuwa na sifa hatutasita kufanya hivyo. Kwa hiyo hatua zote ambazo tume itatushauri hatutasita kufanya hivyo,” alisema.

Rais Samia alisema anatambua uwepo wa ripoti za tume mbalimbali ikiwemo ya mwaka 2013, akisema uchunguzi unaofanywa utazingatia pia mapendekezo ya tume hiyo.

Miongoni mwa mambo kamati hiyo inatarajiwa kukutana nayo, ni ghorofa nyingi katika eneo la Kariakoo kugeuzwa maghala ya kuhifadhia mizigo ya wafanyabiashara, jambo linaloongeza uzito kwenye majengo husika, kwani yapo yaliyojengwa kwa ajili ya makazi pekee.

Mwananchi limeshuhudia majengo mengi  yakiwa na maduka ghorofa za chini, huku za juu, ambazo zilikuwa kwa ajili ya makazi zikitumika kama maghala.

Mfanyabiashara na mkazi wa Kariakoo tangu mwaka 1996, Hamad Abdallah amesema majengo yaliyopo ni ya zamani ambayo hayakukusudiwa kwa biashara nzito au maghala makubwa, lakini mahitaji ya sasa yameyafanya kubeba mizigo mizito isiyolingana na uwezo wake kiufundi.

“Kwa sasa asilimia kubwa ya majengo ya Kariakoo hayakaliwi na watu, wenye nyumba wamebadilisha matumizi kuwa maghala na katika uingizwaji wa mizigo, yanakuja malori makubwa yenye futi 40, mizigo yote inapandishwa juu ya majengo haya,” amesema Hamad.

Jambo jingine ni Kariakoo kuharibiwa kwa ujenzi holela  hata katika maeneo yaliyoachwa wazi kwa ajili ya miundombinu. Baadhi ya chemba za majitaka zimeathiriwa na ujenzi, huku ghorofa zikibanana kiasi kwamba hata magari ya zimamoto inapotokea majanga yanashindwa kupita.

Ni kutokana na hayo, baada ya jengo kuporomoka Novemba 16, aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani twitter) aliandika:

“Kwa sheria za mipango miji ilitakiwa viwanja vinne vya ‘high density’ viunganishwe mbele na nyuma kipatikane kiwanja kimoja kikubwa cha kujenga ghorofa imara yenye ‘basement’ kubwa kupaki magari. Ghorofa inayofunguka kwenye mtaa wa mbele na nyuma awali katika awamu ya tatu ushauri huo wa wataalamu wa mipango miji ulishapuuzwa na viongozi kwa presha ya wawekezaji kwa hiyo ghorofa Kariakoo na kwingineko yanajengwa kiholela kwenye viwanja visivyokidhi vigezo. Pamoja na madhaifu ya usimamizi wa ujenzi kiuhandisi, ni vigumu majengo kuwa imara bila kuwa na eneo la kutosha kujenga kitako yaani ‘base foundation’ stahiki.

“Naendelea kuhimiza kurekebisha kosa hizo. Sasa tunavuna hasara kubwa ya upotevu wa mali, maisha na fursa za ajira na aibu ya kushindwa kusimamia viwango vya ujenzi miaka 63 baada ya uhuru. Naendelea kushauri viwango vya ‘vertical development’ vizingatiwe kuanzia sasa. Tujisahihishe.”

Mfanyabiashara wa Kariakoo, Philipo Sanga amesema ujenzi Kariakoo kwa sehemu kubwa umeziba mitaro ya majitaka na ile iliyokuwa ikipitisha maji ya mvua, hivyo kuleta shida wakati wa msimu wa mvua.

“Mvua ikinyesha mtaa huu wa Nyamwezi, ni kama tupo baharini, hakuna sehemu ya njia ya maji kwa sababu zimefungwa kutokana na ujenzi unaoendelea, lakini pia kwa sasa majitaka yanatoka nje kwa sababu njia zake zimezibwa.

“Mbali na hayo, hata ikitokea ajali ya moto, hakuna njia itakayosaidia watu kujiokoa kwa haraka baada ya kuzibwa njia zote na kujengwa maduka,” amesema.

Mbali ya hayo, kumekuwa na uongezaji holela wa ghorofa kwenye majengo pasipo kujali uimara wa msingi.

Mbali ya hayo, baadhi ya wamiliki wa majengo wamekuwa wakiongeza ghorofa kwa chini ili kupata maeneo ya ama stoo au maduka, hivyo kuathiri msingi wa jengo.

Si hayo pekee, baadhi ya mafundi wanaotumika katika ujenzi hawana utaalamu unaokidhi viwango.

“Ujenzi mwingine ni kunyoosha nondo zilizosalia, wanaongeza jengo lingine na kama hakuna nondo, wanaweka nguzo za chuma na kuanza ujenzi kwa ajili ya kugeuza ghala la kuhifadhia mizigo, kama lilikuwa ghorofa mbili zinaongezeka kuwa tatu,” amesema mfanyabiashara Hamad Abdallah.

“Katika eneo la Kariakoo eneo la chini lina thamani kuliko ghorofani kodi ya juu na chini ni tofauti na ili kuendelea kujipatia pesa juu wanafanya ni stoo na chini wanajenga maduka,” amesema Rashid Ame, mmiliki wa duka Kariakoo.

Mhandisi wa majengo, Milton Nyerere amesema udhaifu wa usimamizi na kutotii sheria, ni sababu ya baadhi ya majengo Kariakoo kujengwa chini ya kiwango.

“Majengo mengi Kariakoo yanajengwa bila kutumia wahandisi au wakati mwingine mhandisi anaanza msingi halafu baadaye mmiliki anakuambia basi, anaenda kutafuta fundi mwingine anakokujua yeye,” amesema.

Milton amesema mtindo huo unatumika zaidi Kariakoo, akieleza wengi wanahofia gharama za ujenzi.

“Kariakoo majengo mengi yamejengwa karibu karibu bila kuangalia msingi wa jengo  moja kama unaweza kuathiri lingine. Mfano, unaweza kukuta mmoja anajenga amechimba msingi wa kina cha chini zaidi. Hiyo inaweza kuathiri jengo la jirani ambalo msingi wake uko juu,” amesema.

Related Posts