Adam anausoma mchezo Azam | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Adam Adam amesema kutokupata nafasi ya kucheza sio kwamba ameshuka kiwango na anaendelea kupambana kupambana kuhakikisha muda wote anakuwa fiti, ikitokea nafasi awe msaada kwa timu.

Adam alisema kipindi anapata nafasi ya kuanza, washindani wake wa namba walikuwa wanakaa benchi, pia kila kocha anakuwa na chaguo lake, lakini jambo la msingi kwake ni kuona timu inashinda na kupata pointi.

“Katika nafasi yangu tunaweza wote tukawa vizuri, ila kocha lazima atamtumia mmoja, kwangu sioni shida, ndiyo maana nasema timu ikishinda ni jambo la msingi, wenzangu wananiambia ni suala la muda kucheza kwani hata wao wameona nina kitu, hivyo najitahidi kulinda kiwango changu.

“Licha ya hivyo, kama mchezaji lazima niwaze, kwani nilitamani kufanya zaidi ya nilichofanya msimu uliopita nikiwa Mashujaa na nilifunga mabao saba na asisti mbili, bado muda upo naendelea kupambana.”

Adam aliyepita timu mbalimbali ikiwemo Al-Wahda Tripoli ya Libya, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, Ihefu, Mashujaa na sasa Azam, alisema soka ni kazi yake na hatarajii kunyoosha mikono juu ya kuashiria kushindwa.

Msimu huu ndani ya Azam FC, Adam hajafanikiwa kumaliza dakika tisini hata kwenye mechi moja huku akiwa hajafunga wala kuasisti.

Katika nafasi yake ya ushambuliaji, anashindani namba na Nassor Saadun mwenye mabao matatu katika ligi na Jhonier Blanco ambaye amefunga moja.

Related Posts