Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Athuman Kilapo (60) kulipa faini ya Sh 200,000 au kwenda jela miaka miwili, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na majongoo bahari yaliyo hatarini kutoweka, yenye uzito wa kilo tatu, kinyume cha sheria.
Pia, mahakama hiyo imetaifisha majongoo hayo na kuelekeza yapelekwe kwenye mamlaka husika.
Kilapo amedaiwa kukutwa na samaki hao ambao Serikali imepiga marufuku kuvuliwa kutokana na viumbe hivyo kuwa katika hatari ya kutoweka.
Hata hivyo, mshtakiwa amefanikiwa kulipa faini na hivyo kuepuka adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Novemba 22, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini baada ya mshtakiwa huyo kukiri kosa hilo katika utetezi wake.
Kilapo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mtoni Mtongani, alikiri shtaka lake baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.
Upande wa mashtaka ulikuwa tayari umetoa ushahidi wa mashahidi wanne.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mhini amesema Mahakama hiyo imemtia hatiani mshtakiwa kama alivyoshtakiwa, hivyo anatakiwa apewe adhabu inayostahiki.
“Kwa kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, Mahakama hii inakupiga faini ya Sh200,000 na ukishindwa kulipa faini hii, basi utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani,” amesema Hakimu Mhini huku akielekeza kuwa majongoo hayo yarudishwe kwenye mamlaka husika.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali.
Mshtakiwa alipopewa nafasi na Mahakama hiyo, aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na alikuwa hajui kama kuna sheria inayokataza kumiliki majongoo hao.
Pia, Kilapo amedai kuwa ana familia inayomtegemea na mama yake mzazi anaumwa ugonjwa wa kansa ya titi, hivyo yeye ndio anayemuuguza.
“Mheshimiwa hakimu na mimi ninaumwa kansa, hivyo naomba mahakama yako inipunguzie adhabu,” amedai mshtakiwa huyo.
Awali, Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele aliiomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa viumbe hao wapo hatarini kutoweka.
“Upande wa mashtaka hatuna kumbukumbu za makosa ya nyuma kama mshtakiwa alishawahi kushtakiwa mahakamani hapa, lakini naomba Mahakama yako itoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria,” amedai Mwakamele.
Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili yaani upande wa mashtaka na upande wa mshtakiwa, Hakimu Mhini alisema amezingatia ombi la mshtakiwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo anamhukumu kulipa faini ya Sh200,000 au kwenda jela miaka miwili.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa alikabiliwa kesi ya jinai namba 8444 ya mwaka 2024 yenye shtaka moja la kukutwa na jongoo bahari.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumiliki samaki hao walio katika hatari ya kutoweka kinyume na kifungu cha 23(1) cha Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003, kikisomwa pamoja na kifungu cha 13(2), 67, 128 na aya (c) ya jedwali la tatu la Kanuni ya Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2009.
Baada ya kukamatwa alipelekwa kituo cha Polisi Bandari kwa ajili ya kuhojiwa na kuandikwa maelezo.
Hata hivyo, Machi 22, 2024 mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama hiyo na kusomewa shtaka hilo.