Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema chama hicho, kitaheshimu na kuzingatia ratiba za kampeni zilizowekwa na mamlaka husika, huku akiwataka viongozi na watendaji wa CCM kwenye ngazi zote kuonyesha mfano katika hilo.
Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ameeleza hayo Novemba 22, 2024 wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Msichoke, Vingunguti jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za kuwanadi na kuwaombea kura wagombea wa chama hicho.
“Nasema hili hadharani kwa sabubu kule Songwe kuna chama kimekurupuka, kulikuwa na ratiba ya ACT-Wazalendo, lakini wao walikwenda na kutaka kufanya mkutano, kukatokea fujo.
“Sitaki kukisemea hicho chama, lakini nimeona niseme, CCM hatutakuwa kama wao kutoheshimu ratiba za kampeni, bali sisi tutakuwa chama kiongozi cha kuheshimu kampeni,” amesema Makalla bila kukitaja chama hicho.
Kauli hiyo ya Makalla imefuata baada ya mkutano wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe uliopangwa kufanyika katika mji wa Mlowo, Novemba 22, 2022, kuzuiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa madai kwamba hawakuwa na ratiba ya kufanya mkutano.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, chama hicho kilialikwa na mwenyeji wake, ACT Wazalendo, kufanya mkutano wa pamoja, lakini polisi walizuia na kuwatanya.
Hata hivyo, baadaye na viongozi waandamizi wa Chadema walijikuta mikononi mwa polisi mkoani Songwe kwa mahojiano wakidaiwa kukiuka utaratibu wa kampeni. Hata hivyo, viongozi hao waliachiwa baadaye kwa masharti maalumu.
Katika mkutano wake wa hadhara, Makalla amesema ratiba za kampeni zimeandaliwa na kila chama, akisema CCM inawaahidi Watanzania kwamba hawatatumia ukubwa wa chama chao, bali watafuata utaratibu ili haki itendeke katika mchakato huo.
“CCM itanadi sera zake pasipo kejeli wala matusi kwa sababu wamedhamiria kufanya siasa za kistaarabu. Naomba wananchi wa Ilala mfanye kampeni nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda ili tushinde kwa kishindo katika uchaguzi wa Novemba 27, 2024,” amesema Makalla.
Makalla amesema baada ya wagombea wao kuibuka kidedea katika uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo, watajengewa uwezo wa namna ya kutekeleza majukumu yao, akiwataka kutenda haki kwa wananchi wote.
Mbunge wa viti maalumu, Janeth Masaburi, amewaomba wananchi wa Dar es Salaam kukipigia kura CCM ili kishinde katika uchaguzi huo, sambamba na kuwataka viongozi wa chama hicho, kutembea nyumba kwa nyumba kusaka kura.
Elivs Charles (CCM), anayewania uenyekiti wa Mtaa wa Butiama, Wilayani Ilala, aliwaomba wananchi wa Vingunguti kumpigia kura kwa wingi ili aibuke kidedea.