Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dk Irene Isaka amesema mfuko huo umeimarika zaidi kiutendaji kwa kuwa wafanyakazi wote wana mikataba ya utendaji na wale waliuokuwa na tuhuma mbalimbali wanaendelea kuchunguzwa.
Dk Isaka amesema hayo Novemba 22, 2024 wakati wa mjadala kuhusu ya utekelezaji wa sheria na kanuni za Bima ya Afya, akisema NHIF imejisafisha, wafanyakazi wamethibitishwa na uchunguzi unaendelea kwa wale wenye tuhuma mbalimbali.
Amesema wameimarisha utendaji wa watumishi wa mfuko huo kwa kuwa wanapimwa kwa namna wanavyowahudumia wananchi na wakipelekewa madai ya viashiria vya udanganyifu, kuna mfumo umewekwa kwa ajili ya kuwagundua.
“Uchunguzi unaendelea kwa wale wenye tuhuma mbalimbali, sasa hivi yakiletwa madai ya mtumishi wetu mwenye viashiria vya udanganyifu, kuna mfumo wa uchakataji madai umewekwa, ni rahisi kugundulika, anasimamishwa kazi,” amesema Dk Isaka.
Amesema wakati mwingine wagonjwa nao wanafanya udanganyifu ikiwemo wale wanaosafisha damu, saratani na kisukari, hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa mifumo ya wanachama imeunganishwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) pamoja na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), hivyo ni rahisi kuwabaini.
Dk Isaka amesema ili kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote wameangalia maeneo mbalimbali ikiwemo la kuwapa elimu wanadau wote ambapo wameanza Oktoba 2024 hadi kufikia mwaka 2025 watawafikia wote.
Pia amesema mifumo ya uandikishaji wa wanachama imeboreshwa na sasa si lazima mtu atumie simu janja kujisajili, bali hata akiwa na simu ya kawaida maarufu kama kiswaswadu, atajisajili.
Kwa mujibu wa Dk Isaka vituo vya afya vya umma na binafsi vilivyosajiliwa ni 14,000 nchi nzima na hadi sasa vilivyounganishwa na mfumo huo ni 7,000.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa sera, utafiti na ubunifu wa Wizara ya Afya, Tumainnel Masha amesema sheria hiyo ilishasainiwa na imeshaanza kutekelezwa, hivyo wanaandaa kanuni kwa ajili ya utekelezaji huo.
Amesema kimsingi kanuni na sheria vinamtaka mwananchi kujiunga kwenye bima ya afya kwa wote, anaweza akajiunga kwenye Mfuko wa Bima wa umma au binafsi ili awe na uhakika wa kupata matibabu kabla ya kuugua.
Masha amesema dhana ya bima ya afya kwa wote inahusisha wananchi wote, hivyo wamewatambua wananchi wasio na uwezo kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wapo milioni 3.5 nchi nzima, lakini wataanza kuwagharamia watu 1.2 milioni.
“Jumla ya Sh173 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kugharamia watu wasiokuwa na uwezo, tutawaingiza kwenye mfumo wa bima ili kupata huduma ya bima ya afya kwa wote,” amesema Masha.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Tamisemi anayeshugulikia Afya, Dk Grace Magembe amesema wamejiandaa na bima hiyo ambapo wamenunua vifaa na vifaa tiba ikiwemo CT-Scan za digitali, ambazo zimepelekwa mikoani.
Kutokana na vifaa hivyo, amesema ikitokea hakuna mtaalamu wa mionzi, zinapigwa picha zinatumwa katika hospitali za kanda au taifa wanasoma na kurudisha majibu kwenye hospitali husika ndani ya dakika 10 hadi 15.
Dk Magembe amesema vituo vilivyo chini ya msingi kama vituo vya afya, zahanati na hospitali za wilaya, kumejengwa majengo ya dharura 80 na 28 ya uangalizi maalumu (ICU) na yote yanafanya kazi.
“Kelekea bima kwa wote tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ambazo ni bora ikiwemo kuzifikia huduma za afya anapohitaji, uhakika wa mwananchi kupata bima bila ya kujifilisika, isitokee mtu anataka bima akaunze nyumba na nguo,” amesema Dk Magembe.