Hekaya za Mlevi: Dar lilikuwa Jiji, sasa ni makumbusho

Dar es Salaam. Namkumbuka marehemu Kikumbi Mwanza Mpango. Kwenye wimbo wake “Mtoto wa Mjini” aliimba “Dar es Salaam yachemka kama bahari, vituo vya starehe huku na huko. 

Ukiwakosa wana Kamanyola pitia Sikinde Ngoma ya Ukae, usisahau Msondo Ngoma, wana Chakachua. Mwendo wa Jongoo na Super Bomboka, Mwenge ya Mashujaa, Kimulimuli, UDA pia, Magereza Mzee Makassy Polisi, Kumbakisa, Wana Kimbunga na UDA pia…” Hilo ndilo lililokuwa Jiji kubwa kuliko mengine katika Afrika Mashariki na Kati.

Lakini tusafiri pamoja tukijifikirisha. Madukani kuna tangazo maarufu lisemalo “Bidhaa iliyokwisha kuuzwa hairudishwi”.

Fikiria umenunua fulana kwa Shilingi Elfu Kumi dukani, lakini ulipoenda kuijaribu nyumbani ukaona haikutoshi sawasawa. Hakika utakaporudi dukani na kutaka mbadala, hata wateja wenzako watakushangaa.

Ni kwa sababu hiyo ni yako, si ya dukani tena. Labla ufikirie kuigawa kwa inayomtosha au kuiuza kwa bei ya mkononi. Ingelikuwa wafanyabiashara wangelikuwa wanakubali kirahisi, basi tungesikia mizozo mingi kwa wauza magari.

Wauza magari mapya hutangaza mauzo ya magari mapya yaliyotembea “0 Kilometa”. Jamaa yangu mmoja alibisha na kusema hakuna Ziro Kilometa: Kwani hiyo gari haikutestiwa baada ya kutengenezwa? Lakini alisahau kuwa magari hupimwa kiteknolojia na kuonesha hitilafu kabla hayajaingia barabarani.   

Na hakuna testi ya kienyeji ambapo gari linalazimika kukimbizwa kwenye milima na mabonde ili kujua uimara wake.

Lakini ili kukuthibitishia uthabiti wa bidhaa unayonunua, wauzaji hukupa dhamana ya bidhaa hiyo. Kwa mfano utakaponunua gari utalitumia kwa mwaka mzima, iwapo litakuletea wenge basi watalihudumia bila gharama za ziada. Sharti ni kwamba lisiwe limepelekwa kupigwa spana kwa fundi yeyote. Kama wenge haliishi basi watakubadilishia na kukupa gari jingine jipya.
Wenzetu sasa wameona mbali zaidi.

Unaweza kutumia gari uliyonunua kwa zaidi ya miaka mitatu, ukalichoka. Unaruhusiwa kulileta tena kwenye duka lililokuuzia, ukabadilisha baada kuongeza au kupunguza fedha kulingana na tofauti ya bei zake. Hapa kuna hesabu kubwa inayotumika; kwanza bei ya gari jipya, pili thamani ya gari lako, tatu umeshalitimba kwa kiasi gani.

Watachukua thamani yake na kutoa uchakavu, kisha utaambiwa uongeze kiasi gani.Kila bidhaa ina uchakavu baada ya matumizi. Ndio maana unauziwa gari la 0 Kilometa kwa bei kubwa, hata hivyo bei itashuka kwa kadiri ya umbali inayotembea.

Lakini usije kufananisha gari ya uswazi iliyokwenda kilometa chache na gari ya kishua iliyokwenda kilometa nyingi. Kumbuka guta la uswazi linabeba mzigo wa “kirikuu”, kirikuu inabeba mzigo wa “kenta”, kenta inabeba mzigo wa lori linalobeba mzigo wa meli.

Wajenzi nao wana namna yao ya kupima ubora wa majengo. Siri ya bei za bidhaa kutofautiana vikubwa kwenye maduka ya uswazi na ushuani inahusiana na majengo. Chumba cha kupanga uswahilini ni cha kulala, ni sebule, jiko na stoo kwa wakati mmoja. Hivyo uchakavu wake unakuwa maradufu kulinganisha na ushuani ambako kila huduma inafanyika kwenye chumba chake. 

Wana Dizimu wenzangu walilalamika sana wakati Mheshimiwa Magufuli anapeleka Makao Makuu ya Serikali kwenda Dodoma. Mimi niliwaza tofauti sana, kwani nilikuwa nikiliona Jiji hili la kale kuwa limeachwa na wakati. Ukiitazama ramani ya Jiji ya wakati wa ukoloni, ilikuwa imejipanga kiasi cha mtu kutopotea anapoelekezwa mtaa au nyumba. Lakini sio sasa ambapo kitongoji kina ramani tofauti kutegemea ni wapi ulikoenda kuitazama.

Maana yangu ni kwamba mijini tunaishi kisanii: Ndani ya kiwanja kuna kiwanja, ndani ya nyumba kuna nyumba, ndani ya chumba kuna chumba. Kwa lugha nyepesi tunasema “ndani ya shimo kuna shimo”.

Fikiria mtu amepanga eneo kwa biashara ya nguo, halafu humohumo anauza maembe. Sasa sijui ni yeye kajiongeza au anachukua bukubuku kwa mpangaji aliyepangishwa na mpangaji. 

Pamoja na kwamba biashara ni kujiongeza, lakini unamwelewaje anayekutangazia: “Nauza sumu ya panya na unga wa lishe”! Au mganga anayeroga na kutibu. Yeye huyohuyo anapiga ramli chonganishi, huyohuyo anatibu kwa mizimu, bado anarudisha mahusiano yaliyokongoroka, tena anagawa utajiri wa pesa za majini na anaunganisha na frimason. Wakati mwingine najiuliza wana roho ngumu kiasi gani hata wasiogope kumpiga mgonjwa mahututi.

Huko kote nilikuwa nazungukazunguka (nading’ukading’uka) tu, picha lenyewe ni hili: Zaidi ya Dar es Salaam. Kariakoo ndio imechoka zaidi. Kila siku inapokea maelfu ya wageni ambao hawaondoki. Ingelikuwa Mwenyezi Mungu ametupa uwezo wa kuona matumbo yetu yamebeba nini, nadhani maisha yetu yangelikuwa mafupi sana. Fikiria unakutana na tumbo la mbangubangu lina panya, la mchina lina chura, la ustaadhi lina kitimoto. Lakini takataka zote hizo zitatoka.

Lakini Kariakoo yetu inakula bila kujisaidia. Inafanana na mlevi asiyekubali kulewa. Unaambiwa ili kukuokoa, Mungu alikutengenezea kuzidiwa. Hata chakula kiwe kitamu kama cha peponi, ni lazima ushibe, na ukibisha utavimbiwa.

Hata pombe inoge kwa kiasi gani, umeumbiwa ulevi, na ukibisha utapindua gari usije ukafa. Kama hatutakuwa waangalifu, Kariakoo itabomoka jengo baada ya jengo. Ukisoma ripotiza Tume ya Mheshimiwa Edward Lowassa, ni bora Jiji hili liwe makumbusho.

Related Posts