Dar es Salaam. Ukosefu wa elimu kuhusu magonjwa ya mishipa ya fahamu, ukiwemo wa kifafa, unatajwa kama moja ya sababu ya wanaotumbuliwa na tatizo kutojitokeza kupatiwa matibabu.
Mbali ya hayo, imebainishwa baadhi ya watu wamekuwa wakiishia kwenda kwa waganga wa kienyeji au kwenye maombi, wakidhani ndugu zao wamerogwa au wana mapepo.
Changamoto nyingine imetajwa kuwa gharama kubwa za dawa kwa wale ambao wameshafikishwa kupatiwa tiba, nayo inakwamisha tiba ya tatizo hilo.
Hayo yamebainishwa Novemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam na wadau wa masuala ya afya, katika mdahalo wa kitaifa kuhusu ustawi wa watu wanaoishi na kifafa.
Akichangia mjadala huo, Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Akili kutoka Wizara ya Afya, Erasmus Mndeme amesema watu takribani milioni 50 wanaishi na ugonjwa wa kifafa duniani na kwa Tanzania takribani 500,000 wanakadiriwa kuishi na hali hiyo.
Mndeme amesema kati ya wanaoishi na hali ya kifafa, asilimia 3.7 pekee ndio waliofika kupatiwa matibabu katika hospitali zinazotoa huduma hizo.
Amesema ukosefu wa elimu ni moja kati ya sababu za baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitali kupatiwa matibabu, licha ya kuwa matatizo hayo yanatibika iwapo mgonjwa atawahi kufika katika vituo vya kutolea huduma.
“Baadhi ya ndugu wa wagonjwa au watoto wenye hali hiyo kutokana na kukosa uelewa wa kutosha huhisi wamepatwa na mapepo au kuhusisha imani za kishirikina, hivyo baadhi yao huenda kuwaona waganga wa jadi,” amesema.
Daktari bingwa wa magonjwa na afya ya akili, Nuruel Kitomary amesema jamii kutokuwa na kukosa elimu ya kutosha kuhusu magonjwa hayo huwanyanyapaa wagonjwa.
Amesema jamii inapaswa kutambua mwenye hali ya kifafa ana haki za kuishi kama watu wengine na anapaswa kuwahishwa kwenye matibabu.
Amewataka wazazi wanaowafungia watoto ndani wakiogopa kutengwa shuleni waache kwa kuwa wana uwezo wa kusoma.
“Kuna haja kwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuunganisha nguvu katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu hali hiyo, ikiwemo namna ya kumsaidia kupitia huduma ya kwanza. Pia kufahamu kifafa kinatibika ila si kwenda kwa waganga bali hospitali,” amesema.
“Asilimia kubwa ya watu wa kifafa wanahitaji madaktari wa saikolojia ili wawabadilishe mitazamo yao ya kutojiamini kutokana na hali waliyonayo,” amesema.
Avelina Saidi, mzazi wa mtoto mwenye hali hiyo amesema wakati mwingine anashindwa kumfikisha hospitali kutokana na gharama za matibabu hasa dawa.
Amesema anatumia kati ya Sh6,000 na Sh7,000 kwa siku kwa ajili ya dawa, huku akiwa hana bima kwa ajili ya matibabu.
Pia amesema amepitia changamoto ya unyanyapaa ndani ya familia na jamii na kusababisha kuachika.
“Tunaiomba Serikali kuweka unaafuu wa gharama katika dawa ikiwezekana zipatikane bure,” amasema.
Mkurugenzi Msaidizi, idara ya magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha inaboresha ustawi wa watu wenye hali ya kifafa.
Amesema kwa kushirikiana na wadau wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii katika ngazi mbalimbali juu ya ugonjwa huo.
Amesema Serikali inasomesha wataalamu ndani na nje ya nchi ili kubobea katika eneo hilo ili kuongeza yao katika upande wa magonjwa ya mishipa ya fahamu ambao kwa sasa nchini hawazidi 20.