Kiongozi wa upinzani Msumbiji aweka masharti ya mazungumzo – DW – 23.11.2024

Rais Filipe Nyusi amemualika Venancio Mondlane ofisini kwake mjini Maputo Novemba 26 baada ya vifo vya watu kadhaa katika ukandamizaji wa polisi dhidi ya maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9.

Mondlane, mgombea wa kujitegemea, anayesema uchaguzi ulichakachuliwa kukipa ushindi chama cha Nyusi cha Frelimo, inaaminika aliondoka nchini kwa hofu ya kukamatwa au kushambuliwa, lakini haijulikani aliko. Amesema katika hotuba aliyoitoa kwenye ukurasa wa facebook, kuwa wako tayari kwa mazungumzo ya kweli na yasiyokuwa na mitego.

Soma pia: Kiongozi wa upinzani Msumbiji aitisha maandamano mengine

Maafisa wamemfungulia mashitaka, ikiwemo uharibifu uliosababishwa wakati wa maandamano ya wafuasi wake, ambayo yamepelekea akaunti zake za benki kufungiwa.

Mgombea wa Frelimo Daniel Chapo
Tume ya uchaguzi ilisema mgombea wa Frelimo Daniel Chapo alishinda asilimia 71 ya kura dhidi ya asilimia 20 ya MondlanePicha: Marco Longari/AFP

Sharti jingine katika waraka huo lililowekwa wazi na ofisi ya Mondlane ni kuwa “mchakato huo wa kisheria lazima usitishwe mara moja”.

Aidha unaweka  wazi mambo 20 ambayo Mondlane anataka katika ajenda ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na “kurejesha ukweli kwenye uchaguzi” na kumfungulia mashtaka yeyote aliyehusika katika wizi wa kura.

Mengine ni kuomba radhi kwa umma na fidia kwa vifo vilivyotokea wakati wa maandamano, pamoja na mageuzi ya katiba, uchumi na uchaguzi.

Mashirika ya haki yanawatuhumu vikosi vya usalama Zimbabwe kwa kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji katika nchi hiyo ambayo imeongozwa tangu uhuru kutoka kwa Ureno katika mwaka wa 1975 na chama cha Frelimo.

Polisi yatawanya waandamanaji kwa gesi ya machozi Msumbiji

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kituo cha Demokrasia na Haki za Binaadamu, ambacho ni shirika la kiraia kinasema karibu watu 65 wameuawa. Mondlane alisema Ijumaa kuwa waliokufa ni zaidi ya 60. Nyusi alisema Jumanne kuwa watu 19 waliuawa, wakiwemo polisi watano.

Rais anapaswa kukabidhi Madaraka Januari mwakani kwa mgombea wa Frelimo Daniel Chapo, ambaye tume ya uchaguzi inasema alishinda asilimia 71 ya kura dhidi ya asilimia 20 ya Mondlane.

Machafuko hayo yalijadiliwa Jumatano na viongozi wa kikanda katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC yenye nchi 16 wanachama, ambayo ilisema katika taarifa baadae kuwa “inatuma salamu za rambirambi kwa serikali na watu wa Msumbiji” kwa vifo vilibvyotokea.

Shirika la haki za Binaadamu la Human Rights Watch Ijumaa liliikosoa SADC kwa kushindwa kuikemea Msumbiji kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi.

AFP

Related Posts