Uyui. Aliyekuwa mgombea wa chama cha ADC katika nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji cha Godawn kilichopo katika kijiji cha Ilolangulu, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Mashaka Said amefariki Dunia Novemba 21, 2024 ikiwa ni siku moja baada ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 ambapo kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali kupitia vyama vyao, zilianza tangu Novemba 20, 2024 na zitadumu kwa siku saba hadi Novemba 26, 2024.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 23, 2024, mtoto wa marehemu, Lintu Mshindo ambaye ni msemaji wa familia, amesema baba yao alifariki Novemba 21, 2024 baada ya kuugua ghafla wakati akiendelea na shughuli zake za kisiasa.
“Baba alikuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji cha Godawn, Novemba 19, 2024 wakati anatoka kwenye matembezi yake, ndipo alianza kuumwa na baadaye tukampeleka kituo cha afya, kata ya Ilolangulu ambapo kutokana na hali yake kuwa mbaya, walitupatia rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Tabora (Kitete),” amesema.
Hata hivyo, Mshindo amesema baada ya baba yake kupokelewa mapokezi katika hospitali ya Kitete, alilazwa huku akilalalamika miguu yake kufa ganzi pamoja na tumbo kuuma, baadaye hali ikawa mbaya, akahamishiwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU) ambapo alikaa kwa muda wa saa tano, akipatiwa matibabu na bahati mbaya akafariki wakati akitibiwa.
Mshindo amesema baba yao alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ngiri, ambao alikuwa nao kwa muda mrefu na kwamba hajafariki kwa sababu za kisiasa.
Akizungumzia kifo hicho, diwani wa kata ya Ilolangulu (CCM), Wilaya ya Uyui, Mohamed Linsu amesema wameshtushwa na kifo cha mgombea huyo ambaye alikuwa mtu wa watu katika kata hiyo.
“CCM) tumesikitishwa na kifo cha mgombea huyu wa nafasi ya uenyekiti kwenye kitongoji cha Godawn ambaye tunakiri ya kwamba alikuwa mtu wa watu na tumepoteza mtu muhimu kwenye jamii yetu. Alikuwa mpenda watu, hivyo tunaiombea familia kwenye kipindi hiki kigumu kwao,” amesema.
Linsu amesema inapotokea mgombea wa nafasi ya uenyekiti kafariki dunia, basi uchaguzi kwenye kitongoji husika utaendelea kwa nafasi zingine kama wajumbe kuchaguliwa kama kawaida, lakini nafasi ya uenyekiti lazima atafutwe mgombea atakayeziba pengo.
Kamishna wa ADC Mkoa wa Tabora, Ramadhan Said amesema chama hicho kimepata pigo kubwa kumpoteza mgombea huyo.
“Tumesikitika sana kama chama kuondokewa na mgombea wetu, alikuwa mtu makini na kama sio umauti kumfika, tunaamini kwamba angeshinda uchaguzi na kuwa kiongozi kwenye kitongoji alichokuwa akigombea,” amesema Said.
Hata hivyo, Kamishna huyo amesema baada ya mgombea wa chama chake kupoteza maisha, wameshapewa barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi inayoeleza kusimamisha uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti na kwamba baada ya siku 40, ADC kitatakiwa kuteua mgombea mwingine kwa ajili ya kuendelea na uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti.