MWANDISHI WA SUAMEDIA AIBUKA MSHINDI WA TUZO YA MWANDISHI BORA WA SAYANSI KIPINDI CHA MUONGO MMOJA

 

Na Mwandishi Wetu

Mwandishi wa habari za sayansi kutoka SUAMEDIA Calvin Edward Gwabara ameibuka mshindi wa tuzo ya Mwandishi Bora wa  Sayansi Tanzania katika kipindi cha Muongo mmoja katika kuelekea Kongamano la Kitaifa la Sayansi Teknolojia na ubunifu linalotarajiwa kufanyika tarehe 2-4 Desemba Jijini Dar na kufunguliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tuzo hiyo imetolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH kupitia Jukwaa la wazi la Bioteknolojia afrika (OFAB) na kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni COSTECH, Prof. Makenya Maboko mbele ya Wahariri wa Vyombo vya hahari nchini hafla iliyofanyika kwenye ofisi za tume hiyo jijini Dar es salaam.

Tuzo hiyo imetolewa kwa  kutambua mafanikio bora na kujitolea kwake katika uandishi wa habari za Sayansi kwa kuripoti kwa ufanisi na  bila kuyumba na kwa  ukweli na ubora unaovutia katika   eneo la uandishi wa habari za sayansi nchini Tanzania.

Wengine waliopata Tuzo ni Watangazaji watatu wa Kipindi cha Redio cha Uhuru FM  Kwa pamoja kwa kufanya kipindi bora cha Sayansi pamoja na Katibu Mkuu mstaafu Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Dkt. Omar Shajack ambaye ameibuka kuwa Champion wa Bioteknolojia Tanzania

Akizungumza kwenye Mkutano huo mbele ya Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF na Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt. Amos Nungu amesema tuzo hizo zimetolewa kwa kutambua mchango wa Vyombo vya habari na Wanahabari katika kutangaza na kuhabarisha Umma kuhusu kazi mbalimbali za Saysnsi teknolojia na Ununifu.

“ Tunatoa Tuzo leo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Kongamano kubwa la Sayansi Teknolojia na Ubunifu ambalo linaenda sambamba na Maonesho linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 2- 4 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mwl Nyerere jijini Dar es salaam ambalo Mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” Alisema Dkt. Nungu.

Amesema kongamano hilo la mwaka  2024 litahusisha Watafiti, Wabunifu, Watunga sera na wadau wote wa Sayansi ambapo mambo kadhaa yatazinduliwa na Rais Mhe. Samia ikiwemo uzinduzi wa dirisha la mikopo ya gharama nafuu Kwa wabunifu, Utoaji wa Hundi kwaajili ya maandiko ya utafiti 19 yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 6.3 pamoja na kuwashika Mkono watafiti ambao tafiti zao zimeleta tija kubwa kwa Taifa.

 

Related Posts