Nchimbi ataka viongozi wasifunike mazuri ya watangulizi wao

Morogoro. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka viongozi wanaopata dhamana katika nafasi mbalimbali wasisahau au kupuuza yaliyofanywa na watangulizi wao.

Amesema ili jamii na Taifa lipige hatua viongozi wanapopata madaraka ndani na nje ya serikali kuhakikisha wanaenzi na kutambua michango ya waliokuwapo kwenye nafasi hizo.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumamosi, Novemba 23, 2024 katika Mkutano Mkuu wa 24 wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe. Alikuwa mgeni maalumu.

Mahafali yatafanyika kesho Jumapili Novemba 24 chuoni hapo, mgeni maalumu akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyewahi kusoma Mzumbe.

Dk Nchimbi amesema hayo alipomzungumzia Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Mwegoha ambaye kitaaluma ni mhandisi.

Amesema baada ya Profesa Mwegoha kuteuliwa kushika wadhifa huo, ameendeleza pale watangulizi wake walipoishia.

Dk Nchimbi amesema jana Ijumaa Novemba 22, alipata fursa ya kuzungumza kwa kina na Profesa Mwegoha na kubaini ameendeleza misingi ya kuanzishwa kwa chuo hicho ambacho kimezalisha viongozi mbalimbali akiwemo, Rais Samia.

“Watu wengine wakipewa madaraka kwenye fani tofauti na za kwao anaanza kuwalazimisha wenzake wamfuate, lakini makamu mkuu wa chuo chetu licha ya kuwa mhandisi ameendeleza tamaduni ya chuo chetu,” amesema.

Akisisitiza hoja hiyo, Dk Nchimbi amesema: “Kuna watu wakipewa madaraka wanafuta kila kitu kilichoanzishwa na wengine, ni kiwango kikubwa cha ujinga.”

Hoja hiyo imeungwa mkono na Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu ambaye amesema Profesa Mwegoha ameendeleza falsafa, maadili na utamaduni wa Mzumbe kwa kuzalisha wasomi wenye nidhamu na weledi.

Kingu ambaye ni mhitimu chuoni hapo amesema mfano mwingine ni Rais Samia ambaye baada ya kuingia madarakani Machi 19, 2021 hajafuta ya mtangulizi wake hayati Dk John Magufuli.

“Rais Samia ameendeleza miradi iliyoachwa na hayati Magufuli na kuanzisha mingine. Huu ndio uongozi, kutambua yaliyofanywa na mtangulizi wako si kuyaacha au kuyaona hayana maana.

“Kila mtu anapokuwa kiongozi ana umuhimu wake, si vizuri au jambo jema unapoingia kwenye nafasi yoyote kuyapuuza ya mtangulizi wako.”

Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi amezungumzia suala la ajira akisema dunia tunayoishi leo inapata mabadiliko makubwa yasiyoweza kufananishwa na kipindi chochote cha nyuma.

“Kila sekta, kila tasnia, na kila soko la ajira linabadilika kwa namna ambazo hatungeweza kufikiria miaka 10 iliyopita. Kuongezeka kwa matumizi ya akili bandia (mnemba), umuhimu wa uchumi wa kijani, na mapinduzi mapya ya kiteknolojia vinaendelea kubadili sura ya kazi,” amesema.

Dk Nchimbi amesema njia ya kazi za jadi inabadilika, nyingine zinapotea na milango mipya inajitokeza.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza katika mkutano mkuu wa 24 wa Baraza la Wahitimu la Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mkoa wa Morogoro. Picha na Mpigapicha Wetu.

Amesema hali hiyo inayobadilika kwa haraka inatoa changamoto kubwa na fursa zisizo na kipimo kwa wahitimu, huku wakiingia kwenye soko la ajira.

“Dunia inahitaji si tu wafanyakazi, bali viongozi jasiri ambao watakuwa mstari wa mbele katika mabadiliko haya,” amesema.

Dk Nchimbi amesema elimu imekuwa daima ni kichocheo cha nguvu ya mabadiliko.

“Hapa Mzumbe hamjapata tu maarifa ya maana bali pia mmejenga uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, na kuleta ubunifu.

“Katika enzi hii ambayo mabadiliko ni ya mara kwa mara, wito si tu wa kujirekebisha leo, tunahitaji mwongozo wenu katika mabadiliko haya. Hamtoki tu katika dunia jinsi ilivyo, mnatakiwa kutengeneza dunia inavyoweza kuwa. Chuo Kikuu cha Mzumbe kimewaandaa kwa changamoto hii, na sasa ni zamu yenu kuangaza,” amesema.

Kuhusu ujasiriamali, Dk Nchimbi amesema ni muda mrefu Taifa limekuwa likitegemea mifumo ya ajira za kitamaduni kama njia pekee ya mafanikio jambo ambalo kwa sasa limebadilika.

Amesema ni wakati sasa wa kutafakari upya fikra hizo, kwamba mustakabali wa uchumi wa Tanzania hauko tu kwenye kujaza nafasi zilizopo katika kampuni, bali uko katika kuunda fursa mpya, tasnia mpya, na biashara mpya.

“Nawahimiza kila mmoja wenu kufikiria changamoto si kama vikwazo bali kama fursa za kuunda ajira. Nguvu ya kuunda mustakabali wa kiuchumi wa Taifa letu iko mikononi mwa akili bunifu na za kijasiriamali kama zenu. Mawazo yenu, dhamira yenu, na ujasiri wenu ndiyo yatakayotufanikisha,” amesema.

Awali, rais wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Ludovick Utouh amesema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho kikianza kama Taasisi ya Maendeleo Mzumbe (IDM) imezalisha wasomi wengi wanaolitumikia Taifa ndani na nje ya Serikali.

Amesema miongoni mwao ni Rais Samia ambaye kupikwa kwake vyema chuoni hapo ndiyo matunda anayoyafanya sasa ya kuwa kiongozi bora kwa kuifanya nchi kuwa sehemu salama.

Wengine amewataja ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, ambaye ameeleza mafunzo aliyoyapata chuoni hapo yamemfanya kuendelea kuaminiwa kwa kuteuliwa kwenye tume mbalimbali, zikiwemo za Haki Jinai na ya Maboresho ya Mifumo ya Kodi.

Pia mawaziri waliokuwapo kwenye kongamano la wahitimu na mkutano wa mwaka wa baraza hilo ambao ni Balozi Pindi Chana (Maliasili na Utalii), Anthony Mavunde (Madini) na Dk Ashatu Kijaji (Muungano na Mazingira).

Wapo pia wabunge ambao ni Kingu (Singida Magharibi) Japhet Hasunga (Vwawa) na Subira Mgalu (Viti Maalumu).

Utouh ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, amewaomba wahitimu wote wakiwamo mawaziri, wabunge, mabalozi na wafanyabiashara kuendelea kuwa mabalozi wema huko walipo, wakikumbuka kuchangia kwa chochote kwenye mfuko wa kusaidia masomo kwa wanafunzi.

Utouh ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu amesema wahitimu wakaitumie elimu waliyoipata kwenye maisha yao.

“Tunajifunza kwa ajili ya maendeleo ya watu,” amesema.

Pia amewataka wanafunzi, hususani wahitimu kujielekeza kwenye ujasiriamali ili kupambana na adui umasikini na tatizo la ajira.

Amewataka kuzingatia misingi mitatu ya uaminifu, kufanyakazi kwa bidii na juhudi, pindi wanapokuwa katika ujenzi wa Taifa.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Mwegoha amesema suala la usawa wa kijinsia limepiga hatua akitoa mfano, wahitimu wa mwaka huu ni takribani 50 kwa 50 akieleza asilimia 50.2 ya wahitimu ni wanaume na asilimia 49.7 ni wanawake.

“Naweza kuona jinsi tunavyopiga hatua kwa vitendo,” amesema.

Related Posts