Songwe. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake wakiachiwa kwa dhamana, kada wa chama hicho, Mdude Nyagali ameendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.
Jana, Novemba 22, 2024, Mbowe na wenzake 11, akiwamo Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Songwe, kwa madai ya kutaka kufanya kampeni eneo lisilostahili, ikiwa ni kinyume na kanuni na taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, viongozi hao waliachiwa kwa dhamana wakitakiwa kuripoti tena kituo cha Polisi mkoani humo, Alhamisi Novemba 28, 2024 kwa mahojiano zaidi.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 23, 2024, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Agustino Senga amesema baada ya mahojiano na viongozi hao, wameachiwa kwa dhamana na masharti maalumu huku wakibaki na Mdude Nyagali.
Amesema wanamshikilia Mdude kwa ajili ya kuhojiana naye kuhusu mambo mengine yanayomkabili.
“Wito wangu ni uleule kwa vyama vya siasa hasa viongozi, kuzingatia utaratibu wa kampeni kwa ratiba zilizopangwa, hatutasita kuchukua hatua.
“Tunahitaji kuona uchaguzi ukienda vizuri kwa amani na uhuru kama kanuni zinavyoelekeza. Sisi sote ni Watanzania, uchaguzi ni wetu sote na wananchi wana haki ya kikatiba, tufuate utaratibu,” amesema Senga.
Amesema mtu kufanya mkutano eneo lolote bila kufuata utaratibu ni dalili za kuleta vurugu, amewaomba viongozi na wananchi kufuata ratiba huku akieleza kuwa jeshi hilo lina ratiba zote za vyama.
“Wananchi wenyewe wanafuata wanachoambiwa na viongozi wao kwamba waje sehemu fulani, hivyo tunaomba viongozi wazingatie ratiba na Jeshi la Polisi tunazo ratiba za vyama, kufanya mkutano eneo ambalo si sahihi ni dalili za vurugu,” amesema kamanda huyo.
Akizungumzia kuhusu hali za majeruhi wakati wa makabiliano kati ya makada wa Chadema na polisi, Senga amesema askari wawili na raia mmoja waliojeruhiwa wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.
“Majeruhi wote wametibiwa na kuruhusiwa, isipokuwa askari mmoja aliyejeruhiwa sehemu za usoni, bado anapatiwa matibabu,” ameeleza Senga.