Mbeya. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabuni amewataka viongozi wa dini ya Kikristo nchini, kuungana na kuanzisha programu maalumu ya mitaalaa ya elimu ya mafundisho ya Biblia kuanzia elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kulinda maadili kwa vijana.
Amesema kuanzishwa kwa masomo hayo kuende sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya uchapaji na ugawaji wa Biblia bure, zenye mtaalaa mmoja wa kufundisha baina ya dhehebu moja na jingine na kutoa ajira kwa walimu wa dini nchini.
Profesa Kabudi ametoa wito huo leo Jumamosi, Novemba 23, 2024 alipokuwa mgeni rasmi wakati wa ibada ya kumweka wakfu Askofu mteule wa Kanisa Baptisi Kanda ya Kusini Magharibi, Mchungaji Sylvester Mbwaga.
“Nasema hivyo kwa sababu dunia imebadilika kutokana na kukua kwa teknolojia za utandawazi, hali inayosababisha watu kufika mbali kwa kuamini Mungu hayupo jambo ambalo sio sahihi,” amesema.
Profesa Kabudi amesema lengo la kusisitiza uanzishwaji wa mitalaa ya elimu ya Biblia shuleni ni kuokoa vijana kuporomoka kimaadili na kuingia kwenye upepo mbaya.
“Suala hilo halina mjadala wala kuhitaji ufadhili, nendeni muweke mikakati ya uanzishwaji wa mitalaa sambamba na elimu ya masuala ya familia na ndoa,” amesema.
Wakati huohuo, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa kushirikiana na uongozi wa kanisa hilo kuanza mchakato wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Uhai Baptisti kuwa hospitali ili kuboresha huduma kufuatia ombi lililotolewa kwake.
“Uhai Baptist ni zao la Hospitali ya Rufaa Kitengo cha Wazazi Meta kabla haijawa chini ya Serikali, tunatambua mchango wenu ombi lenu la kupandishwa hadhi, nimetoa maelekezo kwa ngazi ya mkoa,” amesema.
Profesa Kabudi amewataka viongozi wa dini kuombea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 na kuhamasisha waumini kupiga kura kuchagua viongozi watakaokuwa chachu ya kuleta maendeleo.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Anord Manase amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kuvutana, bali watambue uongozi ni kipawa kutoka kwa Mungu.
“Uongozi wowote ni kipawa ambacho Mwenyezi Mungu kamwandalia mwanadamu, sio vita wala kuingiza tamaa katika uongozi,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewataka viongozi wa dini kuendeleza amani katika Mkoa wa Mbeya, pia, amewataka waumini kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa ili kupata viongozi wawatakao kwa maslai ya Watanzania.
“Hamasisheni waumini kushiriki chaguzi zilizo mbele yetu pamoja na kuwa waumini wazuri wa kujenga imani ya kujikita katika shughuli za kiuchumi ili kujikwamua kiuchumi,” amesema.
Muumini wa kanisa hilo, Chuma Amos amesema watashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.