Serikali: Sera ya Bima ipo hatua za mwisho kukamilika

 

SERIKALI imesema kuwa ipo mbioni kukamilisha sera itayoiongoza sekta ya Bima nchini ili kuendeleza usanifu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa jana tarehe 22 Novemba 2024 na Hamad Chande, Naibu Waziri wa Fedha wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utendaji wa Bima nchini ya mwaka 2023.

Naibu Waziri Chande amesema kuwa serikali ipo katika hatua nzuri za kukamilisha utungaji wa sera.

Amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa mfumo wa madai na isikilizwaji wa malalamiko kwenye mifumo ya bima.

“Ukiaminiwa aminika zipo baadhi ya kampuni za bima zimekuwa zikilalamikiwa lakini tunashukuru kwa kuwepo kwa mfumo wa usikilizwaji wa malalamiko ya watu,” amesema Waziri Chande.

Waziri Chande ameipongeza taarifa hiyo kwa kutoa taswira nzuri katika ukuaji wa uchumi wa nchi hususan katika eneo la ongezeko la ajira.

Kamishna wa Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dk. Baghayo Saqware

Bima imeongeza ajira kwa asilimia 34.1 kutoka ajira rasmi 4,173 mpaka kufikia 5,595 kwa mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Mamlaka ya Bima nchini (TIRA), Dk. Baghayo Saqware alipokuwa akitoa ripoti ya mwaka 2023 jijini Dar es Salaam.

Mchango wa Bima kwenye pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.99 kwa mwaka 2022 na kufika asilimia 2.1 kwa mwaka 2023.

Saqware amesema kuwa uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kijikinga kwa kukata bima umeongezeka kwa asilimia 4.4.

“Matumizi ya bima kwa mtu mmoja mmoja yameongezeka kutoka shilingi 18706 kwa mwaka 2022 na kufikia 19531 kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 4.4,” alisema Saqwere.

Amesema kuwa kiashiria cha kukua kwa Bima ni pamoja na kuongezeka kwa malipo ya madeni ya bima kwa asilimia 25.5 kutoka Sh. 389 milioni kwa mwaka 2022 hadi Sh. 488.2 milioni kwa mwaka 2023.

Mali za bima zimeongezeka kwa asilimia 26.8 kutoka Sh. 1,697 bilioni kwa mwakan 2022 hadi kufikia Sh. 2,152 bilioni kwa mwaka 2023.

“Mali za uwekezaji katika bima zimeongezeka kwa asilimia 9.3 kutoka Sh. 1,170 bilioni kwa 2022 kufikia Sh. 1,278 bilioni kwa mwaka 2023,” alisema.

About The Author

Related Posts