Dar es Salaam. Tanzania imeingia mikataba na nchi 88 zenye mashirika ya ndege, ambayo yanaingia na kutoka katika viwanja vya ndege vilivyopo nchini, ikiwa ni sehemu ya kuongeza wigo wa ushirikiano na mashirika ya ndege.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Daniel Malanga amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha inaongeza idadi ya nchi na mashirika ya ndege, yanayoingia nchini kwa kufanya mazungumzo na nchi mbalimbali.
Akizungumza kwenye mkutano wa 44 wa mwaka wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TATCA), Malanga amesema kazi kubwa inafanyika kuhakikisha Tanzania inatanua wigo wa ushirikiano na mataifa mengine katika sekta ya anga.
Amesema mikataba hiyo ambayo kwa mwaka huu imeongezeka zaidi, itafanya mashirika husika kuingia Tanzania na ya nchini kuingia katika nchi husika.
“Miaka mitatu iliyopita tulikuwa na nchi 60 ambazo ndege zao zinatua nchini sasa hivi tumefika nchi 88. Mwaka huu pekee tulisaini mkataba na nchi tatu tukiwa Malaysia.
“Tunafanya hivyo ili kuvutia kasi ya ongezeko la mashirika wapo wanaotutafuta na wengine tunawatafuta kwenye mikutano ili waweze kuja kuwekeza katika sekta hii. Hii itasaidia kukuza sekta mbalimbali za usafiri wa anga ambao ukikua utasaidia kuinua sekta mbalimbali kama utalii, biashara na nyinginezo,”amesema Malanga.
Akizungumzia kuhusu waongoza ndege amesema usafiri wa anga una mihimili mitatu ambayo ni viwanja, mashirika na waongoza ndege hivyo mihimili yote mamlaka inaiangalia kwa ukaribu.
“Katika sekta ya anga ukikosa uimara katika mhimili mmoja huwezi kutoa huduma vizuri, hivyo mhimili wa waongoza ndege leo wamekutana ambapo miongoni mwa mada zilizopo ni pamoja na usalama katika usafiri wa anga,ufanisi,kuendelea kuwepo katika usafiri wa anga,”amesema Malanga.
Amesema mkutano huo umewakutanisha waongoza ndege katika nchi mbalimbali ikiwemo zikiwamo Uganda, Kenya, Burundi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) lengo ni kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo.
Kwa upande wake rais wa TATCA Merkiory Ndaboya amesema pamoja na mafanikio mbalimbali, kumekuwa na changamoto nyingi hasa ya watalaamu.
Amesema kwa sasa nchi ina jumla ya waongoza ndege 143 huku uhitaji ukiwa ni 160.
“Hali ya watalaamu wa taaluma hii sio nzuri,bado watalaam hawatoshi kwa sababu ni sekta inayokua haraka,”amesema.
Mbali na kuwapo kwa wahudumu hao kwa mwaka huu mamlaka imetoa mafunzo kwa vijana 17, ambao wataongeza idadi ambayo bado itakuwa ndogo kwa kuwa viwanja vinafungiliwa vya ndege na sekta inakua haraka.