TWENDE NA KASI YA DUNIA UBUNIFU NA UJASIRIAMALI: BALOZI NCHIMBI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kuendelea kuwa viongozi wa mabadiliko katika soko la ajira la Tanzania, wakienda sambamba na kasi ya dunia katika maeneo ya ujasiriamali na ubunifu.

Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu ya Morogoro, Balozi Nchimbi amesema ni muhimu kwa vyuo vya elimu ya juu na wahitimu wake kuzingatia kasi ya mabadiliko ya dunia katika maeneo ya ubunifu, ujasiriamali, na uongozi ili kuleta mapinduzi makubwa katika kutengeneza fursa za ajira nchini.

Kupitia mkutano wa baraza hilo uliofanyika leo tarehe 23 Novemba 2024, ukiwa na kauli mbiu isemayo “Kuwawezesha wanafunzi kufanya mapinduzi katika soko la ajira na kuchochea upeo mpya wa fursa za kazi,” Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa mapinduzi hayo, mbali ya kusaidia kutengeneza fursa za ajira, kujiajiri na kuajiriwa, pia yatakuwa sehemu ya misingi ya kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Maendeleo ya teknolojia, masuala ya akili bandia, na uchumi wa kijani vimekuwa vichocheo vikubwa vya mabadiliko duniani. Sisi Watanzania, kipekee wahitimu wetu, wanapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa ufanisi. Ninatoa wito kuhusu umuhimu wa kutambua umuhimu wa ubunifu katika kutatua changamoto, kwa kuzingatia maslahi ya taifa,” amesema Balozi Nchimbi.

Alisema kuwa dunia inabadilika haraka, hivyo ni muhimu kwa wahitimu kuchukua fursa hizo ili kuleta maendeleo endelevu, huku akiwasisitiza kutumia elimu waliyoipata chuoni hapo, kuwa sehemu ya kutafuta njia za kuboresha masoko ya ajira kupitia matumizi ya teknolojia na ubunifu, na kushiriki kwa dhati katika mchakato wa maendeleo.

Katika hotuba yake, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kutengeneza fursa za ajira na maendeleo ya vijana, kwa sababu kundi hilo ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Aidha, alisisitiza kuwa sekta ya ujasiriamali, ni mojawapo ya sekta zitakazosaidia kufungua fursa za ajira na kukuza viwanda na biashara mpya nchini. Aliwahimiza wahitimu kuwa na mtazamo wa kimataifa na kuona changamoto kama fursa za ubunifu na maendeleo.

Balozi Nchimbi pia alizungumza kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika maendeleo ya taifa. Alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanapata fursa sawa katika sekta zote, na aliwahimiza wahitimu wa kike na wa kiume kujitahidi kutimiza malengo yao kwa usawa na kushirikiana kwa pamoja katika kuleta maendeleo.

Balozi Nchimbi pia alitoa wito kuhusu umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wahitimu, wakijifunza kwa watangulizi wao, hasa katika kuunda mitandao ya kijamii itakayosaidia kubadilishana uzoefu na kuendelea kujifunza masuala mapya, ikiwemo mbinu za kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Related Posts