HABARI za uhakika kutoka ndani ya Simba, zinasema kuna kazi ngumu ya kufanya mbele nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Tshabalala ambaye ni tegemeo Stars, amekuwa akicheza kikosi cha kwanza katika misimu 10 mfululizo na alipoletewa washindani wa namba, ikashindikana kumuweka benchi, ikiwemo Gadiel Michael aliyekiri ni beki bora, ila kutokana na kiwango chake ilishindikana kumchomesha mahindi.
Katika misimu 10 aliyocheza Tshabalala wamepita makocha mbalimbali ambao wote wamemtumia kikosi cha kwanza, ambao ni Zdravko Logarusic (2014), Goran Kopunovic (2015), Dylan Kerr (2016), Jackson Mayanja (2016), Joseph Omog (2017).
Habari zinasema uongozi wake umeshaweka bayana fungu wanalotaka ili staa huyo aongeze mkataba Msimbazi na kuna klabu tayari ziko tayari kutoa furushi hilo ambalo Simba wametikisa kichwa na kuna dalili wasilitoe.
Mwanaspoti linajua wamewapa masharti endapo viongozi wakihitaji aendelee kusalia kikosini hapo, watatakiwa kuvunja benki.
Pierre Lachantre (2018), Patrick Aussems (2019), Sven Vandenbroeck (2021), Didier Gomez (2021), Pablo Franco (2022), Roberto Oliveira (2023), Abdelhak Benchikha, Juma Mgunda na sasa Fadlu Davids.
Kwa uthibitisho wa makocha hao kumtumia Tshabalala inaonyesha umuhimu wake kikosini, jambo ambalo linaendelea kuwasua kichwa, ingawa taarifa za ndani, zinasema kuna mgawanyiko wa viongozi, wengine wanataka asepe, huku baadhi waking’ang’ania abakie.
Dau linalotajwa anahitaji staa huyo na wasimamizi wake ili aongeze mkataba mwisho wa msimu ni Sh. 700 milioni kwa Simba, huku ikidaiwa kuna mazungumzo mazuri dhidi ya menejimenti yake na matajiri wa Kaizer Chief ya Sauzi na JS Kabylie ya Algeria.
Kitita cha fedha anachokihitaji beki huyo mzoefu huenda ukawa ndio mwisho wake ndani ya kikosi hicho kutokana na baadhi ya viongozi kukiri kuwa ni fedha nyingi kama wanaomsimamia wasipokubali kulegeza, watajiandaa na maisha bila staa huyo huku wakimuandaa nyota wa kigeni Valentino Nouma ambaye ameanza kupata namba kikosini.
Tshabalala ifikapo Januari mwakani atakuwa amebakiza miezi sita ya kuitumikia Simba na tayari uongozi umeanza mchakato wa kumalizana naye kabla ya msimu haujaisha lakini mlima ni mrefu kwao.
Mwanaspoti lilipomtafuta Meneja wa beki huyo, Carlos Sylivester alisema kwa kifupi kuwa kwasasa hakuna timu ambayo inaruhusiwa kufanya mazungumzo na beki wake kwa vile ni mchezaji halali wa Simba kwa mujibu wa mkataba.
Kwa mara ya kwanza nyota huyo alijiunga na Simba Juni 2014 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba baada ya awali kuchezea pia akademi ya Azam FC.
Kwasasa ana miaka 10 ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi na amekuwa na ubora uleule wa kiwango chake licha ya kuletewa wachezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ila wamechemka mapema na kumuacha nyota huyo akiendelea kupeta.