VIDEO: Mbowe, Sugu na wenzao waachiwa huru

Dar es Salaam. Baada ya kushikiliwa kwa saa 12 na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake 11 wameachiwa huru.

Mbali ya Mbowe, wengine ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Pascal Haonga (mbunge wa zamani wa Vwawa), Apporinaly Boniface ( Mkuu wa Kitengo cha Digital- Chadema), Paul Joseph  na Calvin Ndabila ( maofisa  Habari wa Kanda ya Nyasa).

Pia wamo Khalfan Mbwire, Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wanya  (walinzi wa Mbowe), mwenyekiti wa ACT-Wazalendo mkoa wa Songwe, Ezikia Zambi.


Mbowe asimulia walivyodakwa

Wote hao walikamatwa na jana Ijumaa Novemba 22, saa saba katika mchana katika  Pori la Halungu wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe, Augustino Senga,  Mbowe na wenzake, walishikiliwa kwa madai ya kukiuka utaratibu wa kampeni, wakitaka kufanya mkutano eneo ambalo hawakupangiwa.

Akizungumza jana Ijumaa usiku baada ya kuachiwa,  Mbowe amedai kuwa polisi walizuia mkutano huo ikiwa ni mkakati wa makusudi kuvuruga ratiba za chama hicho maeneo Vwawa, Mbozi na Tunduma.

“Ulikuwa ni mkakati wa makusudi tu, kwa sababu nilikuwa na ziara ya siku moja katika majimbo haya. Hakuna sababu msingi kuzuia, ikizingatiwa vyama viwili kukubaliana kwa kutoa ruhusa kwa chama kingine kufanya mkutano,” amesema Mbowe.

Kwa mujibu wa Mbowe, mkutano wa kwanza ulitakiwa kufanyika Mlowo, ambapo ilikuwa ratiba ya ACT-Wazalendo, ambacho walikubaliana kwamba Chadema kifanye mkutano eneo hilo kwa muda mfupi.

“Cha kushangaza polisi wenyewe wamekuja kuzuia mkutano na kuzua tafrani kwa wananchi waliokuwa wakitaka kufuatilia mkutano huo,” amesema Mbowe.


Mbowe na wenzake walivyokamatwa na Polisi Songwe

Katika taarifa yake, Kamanda Senga amesema askari waliwapa amri ya kutawanyika katika eneo na Mlowo, lakini walikaidi, ndipo polisi walipowatanya kwa nguvu, wakaanza kurusha mawe na kuwajeruhi askari wawili maeneo ya puani, jichoni na kichwani.

Kamanda Senga amesisitizia kwa vyama vyote kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi zinazotolewa na wasimamizi wa uchaguzi ili kuepusha vurugu zinazoweza kuepukika.

Mbowe amewaambia wanahabari kuwa wanatakiwa kuripoti tena kituoni Novemba 29, lakini wanatafakari na kushauriana na wanasheria wa chama hicho, kwa hatua zaidi.

Kwa mujibu wa Mbowe, baadhi ya watu alioambatana nao kwenye msafara amedai wamepigwa.

Related Posts