Viongozi wanavyokimbizana na ratiba ngumu ya kampeni

Dar es Salaam. Zikiwa zimebakia siku tatu kuhitimishwa kwa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, viongozi wa vyama vya siasa wameendelea kupishana katika maeneo tofauti nchini wakiwapigia kampeni wagombea wao kwenye uchaguzi huo.

Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kampeni zake zinazofanyika kwa wiki moja pekee, ambazo zilianza Novemba 20 na zitahitimishwa Novemba 26.

Viongozi wa ngazi za juu wa vyama vya upinzani na wale wa chama tawala wameelekeza nguvu kwenye kampeni hizo, ambazo pia zinaonekana kama njia ya kujiimarisha kwenye majimbo na kata kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwakani.

Nafasi zinazogombewa kwenye uchaguzi huo ni za wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji pamoja na wajumbe. CCM kimesimamisha wagombea katika nafasi zote kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, huku upinzani ukiweka kwenye nafasi 30,977 sawa na asilimia 38 ya nafasi zote 80,430 zinazoshindaniwa.

Licha ya kuwapo malalamiko baada ya wagombea wengi wa upinzani kuenguliwa, viongozi wa vyama hivyo kama ilivyo kwa wale wa CCM, wanaendelea kuchanja mbuga maeneo kadhaa nchini kufanya mikutano ya kampeni kwenye mitaa na vijiji kunadi sera.

Viongozi hao wa kisiasa kutokana na muda uliotolewa wa kufanya kampeni, baadhi wamekuwa wakifanya mikutano kati ya mitatu hadi mitano kwa siku ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Uchaguzi unafanyika kwenye vijiji 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.

Ni kutokana na wingi wa maeneo na muda mfupi wa kufanya kampeni baadhi ya vyama vimekuwa vikiwakusanya kwa pamoja wagombea walio kwenye kata na majimbo kuwanadi kwa pamoja, kisha wahusika kuendelea na kampeni kwenye maeneo yao.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe yupo Kanda ya Nyasa na kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho anafanya mikutano saba kwa siku, akijikita kwenye vijiji na vitongoji kusaka kura kwa ajili ya wagombea.

Akiwa mkoani Mbeya leo Novemba 23, Mbowe pamoja na viongozi waandamizi wa Kanda ya Nyasa wamefanya mikutano katika maeneo ya Ipinda, Mpakani (Kyela), Mpuguso, Kyimo, Ndato (Rungwe) na Kabwe (Mbeya Mjini).

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Tundu Lissu amekuwa akifanya mikutano minne kwa siku, akiwakutanisha wagombea wa uenyekiti wa mitaa, vitongoji na vijiji pamoja kuwanadi kwa wananchi.

Mbowe akiwa Mbeya amesema katika chaguzi zilizopita walikuwa wakifanya vizuri wakiingiza idadi kubwa ya wabunge bungeni, madiwani na wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji lakini uchaguzi uliopita walihujumiwa hadi kubaki bila uwakilishi maeneo yote.

“Kutokana na vipigo tulivyopata, upinzani tulikuwa vyama 19, tukashuka hadi vinne mwaka 2019 na sasa tumebaki vyama viwili, Chadema na ACT-Wazalendo ambao kidogo wanajitahidi kule Zanzibar tofauti na hapa Bara.

“Miaka saba ilikuwa ya vilio, misiba, mahabusu, risasi na maumivu makali hadi baadhi ya vyama vikaamua kupiga magoti kutokana na sera ya CCM waliyoweka kuua upinzani,” amesema Mbowe.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alizindua kampeni za chama hicho mkoani Mwanza. Wajumbe wa kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho wametawanyika mikoani wakiwanadi wagombea wa chama hicho.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla aliyekijita katika majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam alianza kampeni kwa kufanya mkutano mmoja, lakini leo Novemba 23 ameongeza kasi hadi kufikia miwili.

Makalla ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alianza mkutano asubuhi katika jimbo la Kibamba wilayani Ubungo na kumalizia jimbo la Kawe, eneo la Wazo.

Baadhi ya makada wa CCM waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliotubiwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla uliofanyika uwanja wa Msichoke Vingunguti, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, kuanzia leo Jumamosi, Novemba 23 Makalla atakuwa na mikutano miwili kwa siku hadi atakapohitimisha kampeni Novemba 26.

Akizungumza na wananchi wa Kibamba katika mkutano uliofanyika Kimara, Makalla amesema chama hicho hakicheki na mtu katika kushika dola na katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wamejipanga kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.

Amesema kwa sasa CCM kinaendelea na kampeni za uchaguzi katika mikoa yote nchini ili kuhakikisha wanawanadi na kuwaombea kura wagombea wanaopeperusha bendera ya chama hicho tawala.

“Katika uchaguzi huu wa serikali ya mitaa, vijiji na vitongoji tutashinda kwa kishindo, kwa namna chama kilivyojipanga ni sawa na kusema yajayo yanafurahisha,” amesema.

Makalla amesisitiza uchaguzi huo ni muhimu na CCM inauchukulia kwa uzito mkubwa kwa kutambua kazi ya chama cha siasa ni kushika dola, na mchakato wake unaanzia uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kiongozi wa zamani wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyeanza kampeni kwa kufanya mikutano mitatu hadi minne kwa siku, kwa kadri siku zinavyosonga anatarajiwa kufanya takribani 10 kwa siku.

Jumamosi Novemba 23, amefanya kampeni maeneo ya Busunzu Kagezi, Kumsenga, Kizazi, Nyambo, Kibondo Mjini, Rugongwe.

Maeneo mengine ni vijiji vya Kichananga, Magarama, Nyankwi, Kukinama, Nyarugusu, Nyabitaka, Bunyambo na Kibondo Mjini wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema kwa siku amejipangia mikutano minne ili kuwafikia wananchi wa vijijini na vitongojini.

“Leo nimefanya mikutano minne katika vijiji vya Mpunda (kata ya Michelle), Namedi (kata ya Miuta), Nambahu (kata ya Nambahu) na Matogoro (kata ya Tandahimba). Vyote vipo jimbo la Tandahimba,” amesema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema amejiwekea utaratibu wa kufanya mikutano minne kwa siku.

Semu akiwa mkoani Mtwara alifanya mikutano minne katika mitaa ya Kisungule A, Mjimwema, Zahanati na Pachoto, iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Katibu wa Chama cha DP, Abdul Mluya ambaye yupo kijiji cha Lulinza, wilayani Uvinza mkoani Kigoma amesema kwa siku anafanya mikutano mitatu hadi minne ili kuwafikia wagombea wa chama hicho maeneo waliosimamisha.

Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib, ambaye amejikita mkoani Morogoro akiwanadi wagombea, amesema amejiwekea utaratibu wa kufanya mikutano miwili kulingana na mazingira.

“Kadri siku zinavyokwenda tutaongeza hadi mitatu kulingana na mazingira ya eneo husika, lakini pia viongozi wenzangu wanapambana eneo walipo maana tumejigawa kuhakikisha tunafanya kampeni za nyumba kwa nyumba,” amesema.

Related Posts