Dar es Salaam. Mgonjwa mmoja aliyekuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, amenusurika kuchomwa moto (kwa mujibu wa tamaduni za Kihindu) akiwa hai, baada ya uzembe wa madaktari kushindwa kuthibitisha kifo chake.
Mwanaume huyo wa nchini India aliyekuwa akiugua tatizo sugu la mapafu, aliamka muda mfupi kabla ya mazishi yake alipokuwa kwenye tuta la kuchomwa moto.
Rohitash Kumar, mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa akiishi kwenye nyumba ya kuhifadhia watu wenye mahitaji maalumu iitwayo Maa Sewa Sansthan, alikuwa na matatizo ya kuzungumza na kusikia.
Kumar aliugua na kupelekwa hospitalini katika eneo la Jhunjhunu, jimbo la Rajasthan, magharibi mwa India, Alhamisi Novemba 21, 2024 Shirika la habari la AFP liliripoti.
Madaktari walifanyia kipimo cha CPR, lakini waliona mapigo ya moyo wake yakisimama kwenye kifaa cha elektrokardiogramu (ECG) , hivyo kutangaza kuwa alipelekwa hospitalini hapo akiwa ameshafariki.
Hata hivyo, badala ya kufanyiwa uchunguzi wa maiti ili kuthibitisha sababu ya kifo, madaktari katika hospitali ya wilaya ya Bhagwan Das Khetan (BDK) walielekeza moja kwa moja mwili wake upelekwe kwenye chumba cha kuhifadhi maiti.
Baada ya taratibu za maziko kufanyika ikiaminika Kumar ameshafariki aliwekwa
kwenye tuta la mazishi ili kuchomwa kwa mujibu wa mila za Kihindu.
Lakini muda mfupi tu kabla ya moto kuwashwa kwenye tuta hilo, mashuhuda waligundua kwamba alikuwa akijongea, hivyo akaondolewa kwenye tuta hilo na kunusurika kuchomwa moto akiwa hai.
“Hali hiyo ilikuwa muujiza wa kweli. Sote tulishangaa. Alitangazwa kuwa amekufa, lakini pale alikuwa akipumua na hai,” shahidi mmoja kwenye eneo la mazishi aliiambia ETV Bharat.
Gazeti la Times of India liliripoti uchunguzi wa awali ulionyesha madaktari waliripoti kwamba Kumar alishafariki dunia kutokana na tatizo la kupumua kutokana na ugonjwa sugu wa mapafu.
Mkuu wa matibabu wa Hospitali ya Wilaya ya Jhunjhunu, Dk Singh aliiambia AFP kuwa daktari aliandaa ripoti ya uchunguzi wa maiti bila kufanya uchunguzi halisi na mwili ukapelekwa kwenye mazishi.
Hii ilithibitishwa na Ofisa wa afya wa Wilaya ya Jhunjhunu, Ramavatar Meena ambaye aliiambia Times of India kuwa uchunguzi wa maiti ulifanywa kwenye karatasi tu.
Baada ya kuokolewa kutoka kwenye tuta la mazishi, Kumar alirudishwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi cha BDK, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya.
Juhudi zilifanyika kumsafirisha hadi hospitali ya Sawai Man Singh huko Jaipur, umbali wa zaidi ya maili 100 kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo, alifariki dunia wakiwa njiani kuelekea Sawai Man Singh na kutangazwa amefariki.
Madaktari watatu, waliotajwa katika vyombo vya habari vya ndani kuhusika na uzembe huo na kusimamishwa kazi ni mkuu wa matibabu wa BDK, Dk Sandeep Pachar, daktari wa afya ya jamii, Dk Yogesh Kumar Jakhar na Navneet Meel.
Ofisa afya wa Jhunjhunu Meena aliongeza, “huu ni uzembe mkubwa. Hatua zitachukuliwa dhidi ya waliohusika. Mtindo wa kazi wa madaktari pia utachunguzwa kwa kina.”