Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imemhukumu Sifael Kivuyo kutumikia kifungo cha miaka 18 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia Rodgers Kessy aliyemkuta chumbani na mpenzi wa kike wa mwalimu wake wa kuchora.
Ndugu yake ambaye alitajwa kwa jina la Emmanuel Kivuyo alihukumiwa kifungo cha nje mapema kabisa katika hatua za awali baada ya kukiri kosa la kusaidia kuficha taarifa za mauaji hayo, chini ya kifungu 213 cha kanuni ya adhabu.
Awali, Kivuyo alishitakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia, lakini Jaji Lilian Mongella aliyesikiliza kesi hiyo alilishusha kosa hilo hadi kuua bila kukusudia, baada ya utetezi wa Kivuyo kuwa alimuua Rodgers Kessy katika harakati za kujilinda.
Hukumu hiyo iliyopatikana katika Tovuti ya Mahakama Novemba 23, 2024, ilitolewa Novemba 13 mwaka huu huku Mahakama ikimpa faida mshitakiwa licha ya ushahidi wa Jamhuri kudai lengo lilikuwa kumwibia marehemu fedha na pikipiki yake.
Mauaji hayo yalitokea Mei 10, 2021 eneo la Mnazi Shah Tours Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa marehemu ulikutwa na jeraha kubwa kichwani, ambalo polisi walidai lilitokana na kupigwa na nyundo.
Ushahidi wa upande wa mashitaka ulikuwa unadai kuwa, mshitakiwa alimuua Kessy katika harakati zake za kumpora fedha na pikipiki na katika kutekeleza mauaji hayo alitumia waya na nyundo vilivyopokewa kama kielelezo.
Ni ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri kuwa mshitakiwa na Emmanuel Kivuyo, walitaka kuutupa mwili wa marehemu ili kuficha matendo yao.
Utetezi ulioishawishi Mahakama
Katika utetezi wake, Sifael alikiri kumuua Kessy lakini akajitetea kuwa alifanya hivyo katika harakati za kujilinda na kueleza kuwa siku hiyo alikuwa amesafiri kutoka Sanya Juu hadi Moshi kumtembelea mwalimu wake.
Alieleza kuwa, alipofika eneo la kazi la mwalimu wake Elia Laizer ambaye alimpa ufunguo wa nyumba yake na kumtaka aende kupumzika na alipofika, ndipo nje alikuta pikipiki imeegeshwa.
Sifael alifungua mlango na ndani alimkuta mpenzi wa mwalimu wake, ambaye alikuwa na Kessy.
Alieleza kuwa, mpenzi wa mwalimu wake alikuwa hamfahamu ndipo alipomtaka kufahamu yeye ni nani.
Alimweleza ameelekezwa na mwalimu wake kwamba aende hapo kupumzika, na ndipo mwanamke huyo alisema hamfahamu na kumtaka aondoke mara moja katika nyumba hiyo, vinginevyo angepiga kelele kuwa ni mwizi.
Sifael alisema baada ya kuelezwa hivyo, Kessy aliyekuwa na mpenzi wa mwalimu wake, alianza kumshambulia kwa kutumia kioo ndipo alifanikiwa kumsukuma akaangukia nguzo ya chuma ya kitanda.
Baada ya kuona hivyo, yeye na mpenzi wa mwalimu wake walimbia kuondoka eneo hilo, lakini Sifael alienda moja kwa moja kwa mwalimu wake na kumweleza kilichotokea.
Mwalimu wake alimtaka abaki katika eneo lake la kazi pamoja na wafanyakazi wengine ili aende nyumbani kwake, lakini alirejea na pikipiki ya Kessy na kuwaagiza wafunge ofisi na waende kupumzika.
Kwa mujibu wa utetezi wake, mwalimu wake huyo aliondoka na hakujua alikoelekea lakini siku iliyofuata alimpigia simu akimjulisha kuwa amekamatwa na polisi na kumwelekeza afike nyumbani kwa mwalimu wake.
Aliamua kwenda kama alivyoelekezwa, akiwa njiani aliona watu wengi na pembeni kulikuwa na gari la polisi, alimuona mwalimu wake akiwa katika gari hilo la polisi amekalishwa chini.
Alipojitambulisha, polisi walimtaka waende naye kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo na alipokwenda alikataa kutoa maelezo kwa sababu alikuwa peke yake, hapo ndipo alipigwa na kulazimishwa kusaini nyaraka.
Baadaye alipelekwa kwa mlinzi wa amani na kutoa maelezo yake.
Katika hukumu, Jaji Mongela alisema kwa kuzingatia ushahidi wa utetezi wa mshitakiwa, anaona kuwa ni wazi mshitakiwa bado anakiri kumuua marehemu na kwamba katika kesi ya jinai hakuna ushahidi bora kama wa kukiri kosa.
Jaji alisema kwa kuzingatia utetezi wa mshitakiwa kuwa mauaji yalitokana na yeye kujilinda (self defence), swali linabaki ni kama mshitakiwa anahusika na mauaji ya kukusudia au akabiliwe na kosa dogo la mauaji ya bila kukusudia.
“Ushahidi wa Jamhuri ni kuwa lengo lilikuwa kumwibia marehemu lakini kwa upande wa pili mshitakiwa anasema aliandika maelezo kwa mlinzi wa amani yanayoeleza kuhusu ‘self defence’ na hakupewa hayo maelezo,”alisema Jaji.
Jaji alisema kwa kuzingatia mazingira ya tukio lenyewe la mauaji, anaona mshitakiwa ndiye alisababisha kifo cha Kessy lakini kwa kuzingatia utetezi wake, namuona hana hatia ya mauaji ya kukusudia bali kuua bila kukusudia.
Alieleza kuwa, kwa kuzingatia sababu mbalimbali zilizotokana na maombolezo ya mshitakiwa na rai ya upande wa mashitaka, anamhukumu kifungo cha miaka 18, lakini anaondoa miaka mitatu aliyokaa gerezani hivyo itakuwa 15.