Kibaha. Askari Polisi, Austin Kabisana wa Mlandizi, mkoani Pwani amefariki dunia baada ya kugogwa na chombo cha moto wakati akitoka kwenye sherehe ya ‘Send off.’
Sherehe hiyo ya mtoto wa askari mwenzakake ilifanyika jana Jumamosi, Novemba 23, 2024 Kibaha Mjini na wakati akirejea nyumbani alikutana na kadhia hiyo barabara ya Morogoro – Dodoma.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, askari huyo alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani-Tumbi, wakati akiendelea kupatiwa matibabu alifariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Mokas akizungumza na Mwananchi amesema wanaendelea na uchunguzi wa kubaini dereva aliyehusika kwenye ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Amesema mpaka sasa hawajapata uthibitisho wa moja kwa moja kama chombo kilichomgonga askari huyo kilikuwa pikipiki au gari, huku akitoa wito kwa wananchi walioshuhudia tukio hilo kutoa taarifa ili kusaidia uchunguzi unaoendelea.
“Tunajitahidi kufuatilia ili tujue aina ya chombo kilichohusika kama kuna mtu aliyeshuhudia, tunaomba atupatie taarifa kwa namba yetu ili tuweze kufuatilia suala hili,” amesema Kamanda Mokas.
Amesema mwili askari huyo unatarajiwa kusafirishwa kuelekea Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya taratibu za maziko.
Zakayo Sanga, mmoja wa wakazi wa Kibaha, amesema askari huyo atakumbukwa kwa mchango wake katika jamii, hasa kutokana na umaarufu wake katika mchezo wa mpira wa miguu.
Amesema miaka ya nyuma askari huyo alijulikana kwa umahiri wa kucheza mpira wa miguu nafasi ya golikipa na ulimfanya ajulikane na watu wengi.
“Miaka ya nyuma alikuwa kipa maarufu, alishiriki mashindano mbalimbali, na watu wa Kibaha wataendelea kumkumbuka,” amesema Sanga.