Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa tarehe 23 Novemba, 2024 aliungana na Timu ya Organ Troika kushiriki shughuli za uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Namibia ambako Misheni ya Uangalizi ya SADC SEOM iliendelea kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini Namibia.
Balozi Mussa pia alishiriki kikao cha kupokea taarifa ya ufuatiliaji maendeleo ya uchaguzi, ikiwemo mwenendo mzima wa Kampeni za uchaguzi, ambapo timu ya kukusanya taarifa juu ya uangalizi wa uchaguzi na timu ya kukusanya taarifa kutoka katika vyombo vya habari ziliwasilisha taarifa za awali.
Balozi Mussa pia alikutana na kufanya mazungumzo na timu ya SADC Organ Troika inayofanya kazi na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu ya SADC katika Uchaguzi Mkuu wa Namibia uliopangwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wenyeviti wa kamati hizo kutoka Tanzania wamesema maandalizi ya uchaguzi yanaendelea vizuri na kwamba waangalizi wamesambazwa katika vituo mbalimbali, kwa mikoa yote 14 ya Namibia.
Balozi Mussa amewashukuru wajumbe wa timu hizo kwa mwanzo mzuri wa kazi na kuwasihi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwakuwa kazi hiyo ni ya Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ TROIKA) ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu.