Moshi. Uchaguzi wa serikali za mitaa na kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya upinzani kumewaibua viongozi wa dini, huku Askofu Fredrick Shoo akihoji neno huru kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na namna wajumbe wanavyoteuliwa.
Wakati Askofu Shoo akiyasema hayo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima amewasihi viongozi wa dini kutoikubali dhana ya kutenganisha dini na siasa, akidai kuwa kuikubali ni kutotambua wajibu wao.
Kauli za viongozi hao zilitolewa jana Jumamosi, Novemba 23, 2023 mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro katika kongamano la viongozi wa dini kanda ya Kaskazini, ambapo masuala ya uchaguzi na hali ya kisiasa nchini ilionekana kutawala kongamano hilo.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini kupitia miradi ya Norwegian Church Aid, likilenga kujadili umuhimu wa vyombo imara vya kidemokrasia, kulinda haki za binadamu na kukuza ushiriki wa watu katika maamuzi.
Kauli ya Askofu Shoo ambaye ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya (KKKT) ya kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa, imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman kukamatwa huko Songwe.
Mbowe pamoja na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu, mbunge wa zamani wa Vwawa, Paschal Haonga, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Songwe, Ezekia Zambi na wanachama wengine. Walikamatwa Ijumaa Novemba 22 katika pori la Halungu Wilaya ya Mbozi na kushikiliwa na Polisi hadi usiku wa manane walipoachiwa kwa dhamana, huku mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali akiendelea kushikiliwa na jeshi hilo hadi jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga alisema wanasiasa hao wa Chadema walikamatwa kwa kutaka kufanya mkutano wa hadhara eneo lisilostahili ikiwa ni kinyume cha kanuni za uchaguzi.
Viongozi hao wako kwenye kampeni za uchaguzi wa serikali za vijiji, vitongoji na mitaa ambao utafanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza katika kongamano hilo, Askofu Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), aliwataka viongozi wa dini kuungana na kukemea yanayoendelea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa hapa nchini.
“Tumeshuhudia na hata sasa yapo yanayoendelea, kampeni zimeanza tumeona jinsi ambavyo viongozi wa vyama vya upinzani wanavyonyanyaswa, wanavyofanyiwa vurugu, hata sasa hivi ukifuatilia kwenye mitandao yapo yanayoendelea, nasikia Mbowe amekamatwa yaani yaleyale yamejirudia.”
“Ni nani hao wenye mamlaka, wenye hicho kiburi cha kutowasikiliza Watanzania? kutowaheshimu Watanzania tunaposema yale yaliyotokea 2019 na 2020 hatutaki yajirudie na tusingependa yajirudie,” amesema na kuongeza.
“Ni wakati wa viongozi wa dini kusimama, sio kwamba hatuyasemi, tumekuwa tukisema labda kwa sauti mojamoja ya hapa na pale, sasa tuungane kwa pamoja tuseme hatutaki kuona yakijirudia,” amesisitiza Askofu Fredrick Shoo.
Amesema, “kama haya ni katika uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji uchaguzi mkuu ujao (wa Rais, wabunge na madiwani) utakuwa ni wa namna gani,” amehoji Askofu Shoo.
Askofu Shoo, amesema viongozi wa dini walipendekeza masuala yaliyopaswa kufanyika ili kuwepo na tume huru ya kweli akasema, “kwanza ukiangalia kuundwa kwake, kuteuliwa kwake ni nani wawepo katika ile tume, badala yake wameteuliwa watu na limechukuliwa neno ‘huru’ likabandikwa hapo lakini kweli ile tume sio huru.”
Amesema moja ya sababu au kigezo ni nani anawateua, nani anawapa fedha kwani hiyo ndio itaonyesha kama tume ni huru ama sio huru.
“Ndio maana tunasema ikiwa huru, moja ya uhuru ni wasipangiwe bajeti yao na hii isiwe kama kwenda kuomba kwa mtu fulani, hiyo itasaidia katika kujenga uhuru wa tume hiyo, watu ambao wana uzoefu, wazalendo watasimamia uchaguzi katika nchi yetu,” amesisitiza Askofu Shoo.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema, “kama tume ya uchaguzi hii ambayo imebandikwa tu neno huru pale, kwa haya ambayo tumeshaona hapa katika uchaguzi huu, kama ndiyo itakayosimamia uchunguzi mkuu wa mwakani tusitarajie mabadiliko yoyote.”
Kwa mujibu wa Askofu Shoo, wanataka kuona tume huru ya uchaguzi ikiheshimiwa na mabadiliko yakifanyika ili iwe huru kweli itakayosimamia uchaguzi mkuu mwakani na ikiwa na sifa ya tume huru.
“Tumwombee Rais wetu azidi kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi pale anapotakiwa kusimama kama Rais,” amesema Askofu Shoo.
Kuchanganya dini na Siasa
Kuhusu dhana ya kuchanganya dini na siasa, Askofu Shoo amesema tangu zamani taasisi za dini zilitoa sauti yake ya kinabii lakini sasa wanaambiwa waache kuchanganya dini na siasa, akisema hilo sio sahihi hata kidogo.
“Siasa na dini vyote kwa pamoja vina lengo la kutoa huduma kwa mwanadamu. Wanaosema tutenganishe dini na siasa tunafikiri kimsingi ni wale ambao hawajui wala kuelewa maandiko matakatifu yaani Biblia wala Quran,” amesema Shoo.
“Napenda kutoa wito kwa viongozi wote wa dini kuhakikisha kuwa waumini wetu wana ufahamu kuhusu masuala mbalimbali ya mustakabali wa nchi na kamwe tusirudi nyuma au kukatishwa tamaa kwa sababu Mungu amekuweka kuwa kiongozi wa dini kwa kusudi maalum,”amesisitiza Askofu Shoo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Katibu Mkuu TEC, Padri Charles Kitima amewashauri viongozi wa dini kutoikubali dhana ya kutenganisha dini na siasa, kwani kwa kufanya hivyo ni kutotambua wajibu wao kama viongozi wa dini.
Amesema, “kinachotufanya viongozi wa dini tuingie katika siasa ni sisi kupeleka tunu zetu tulizokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kutoka kwenye Biblia na Qur’an, hivyo huwezi kumtenganisha kiongozi wa dini na shughuli za hapa duniani,”
Shoo azungumzia Sh150 milioni za Rais
Askofu Shoo ametumia fursa ya kongamano hilo kuelezea namna viongozi wa dini wanaosimama katika haki na kweli wanavyoweza kuchafuliwa, kuzushiwa na habari zao kupotoshwa ili tu kuwaziba mdomo, masikio na macho.
“Kusimama katika kweli na haki sio jambo la lelemama. Heri wenye kuudhiwa kwa sababu ufalme wa mbingu ni wao kwa sababu alijua katika kutetea haki na kusimama ukweli kuna kuudhiwa”ameeleza Askofu Shoo na kuongeza:-
“Kuudhiwa ili wewe kiongozi wa dini unyamaze. Unapofungua kinywa chako kusema, kukemea, kutetea basi kuna kuudhiwa, na nia ni ili ufunge macho yako, mdomo wako na masikio. Kuna kushambuliwa kwa maneno ya uongo.”
“Kuna kupindishwa kwa maneno uliyoyasema. Kwa mfano juzijuzi nikasoma katika mitandao maneno haya. Shoo na Kitima wakalia kuti kavu. Nikasoma mengine Shoo kapewa hongo ya milioni 150.”
“Nikasema hapa si ningekuwa navaa kiatu na suti safi sana kama ingekuwa ni kweli hivyo. Milioni 150 ambazo zinasemwa Shoo kapewa hongo ni hela sadaka au mchango uliotolewa na mheshimiwa Rais kwa kushirikishwa harambee iliyokuwepo katika usharika wa Freeman Mbowe,” amesema.
“Nazungumzia hapa uwezekano wa kubadilishwa kwa taarifa ili kukufanya Nabii unyamaze ni mkubwa sana. Mahali pengine nikasoma Padre Kitima acha kiherehere chako, unachanganya dini na siasa. Usishangae yanapotokea haya”
Sh150 milioni anazozizungumzia Askofu Shoo kuwa zilichangwa kwenye harambee zilitolewa na Rais Samia kwa ajili ya kuchangia umaliziaji wa ujenzi wa Kanisa la KKKT usharika wa Machame wilayani Hai. Tangazo la Rais kuchangia fedha hizo lilitolewa na Mbowe kanisani hapo kwenye harambee hiyo iliyofanyika Desemba 31,2023 na kuhudhuriwa pia na Askofu Shoo.
“Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshatoa Sh10 milioni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia na familia yake wametoa Sh150 milioni na wameshaweka kwenye akaunti ya kanisa,” alieleza Mbowe katika harambee hiyo.