DC Haniu akunwa jitihada za kuwainua wakulima, wafugaji

Rungwe. Juhudi zinazoendelea kufanywa na taasisi za fedha nchini kupitia huduma za kibenki zilizobuniwa mahsusi kwa wakulima na wafugaji, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu kwa wadau wa sekta hizo, zitasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi miongoni mwao.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Novemba 24, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Jaffar Haniu katika uzinduzi wa kampeni ya ‘Shinda Mechi Zako Kinamna Yako na NBC Shambani’ uliofanyika Tukuyu, wilayani Rungwe.

Kampeni hiyo inaendeshwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mahususi kwa wakulima na wafugaji wa Wilaya za Rungwe na Kyela zote za Mkoa wa Mbeya.

Haniu amesema kuzinduliwa kwa kampeni hiyo kutasaidia kuchochea kasi ya uzalishaji na ukuaji wa uchumi wilayani Rungwe, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Hivyo, amezipongeza taasisi za kifedha nchini kwa jitihada zao za kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wakulima na wafugaji katika kukuza uchumi jumuishi unaochagizwa na huduma rasmi za kifedha.

“Hii ni hatua kubwa sana ikilinganishwa na tulipotoka miaka kadhaa iliyopita, wakulima na wafugaji walikuwa hawaaminiki na taasisi za kifedha kutokana na kutokuwa waaminifu na wengine kutokuwa na dhamana,” amesema Haniu huku akitoa rai kwa taasisi hizo kuendelea kuzingatia riba rafiki kwa wadau hao.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa NBC Tawi la Tukuyu, Erick Mbeyale amesema walengwa wa kampeni hiyo ni wakulima, wafugaji na vyama vya msingi vya wakulima na wafugaji ambao wanahudumiwa na benki hiyo.

“Lengo la kampeni hii ni kuwahamasisha wakulima na wafugaji kutunza fedha zao kwenye mifumo rasmi ya kifedha hasa benki, badala ya kutunza kwenye mifumo isiyo rasmi.’’ Amesema meneja huyo.

Akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya bima mbalimbali zinazotolewa kwa wakulima na wafugaji  kupitia benki hiyo, Meneja Uhusiano Kitengo cha Bima wa Benki ya NBC Kanda ya Kusini, Amani Swilla amesema kupitia huduma hiyo, wakulima na wafugaji wapo kwenye nafasi ya kunufaika kupitia bima za afya, bima ya mazao na bima za vyombo vya moto.

“Kupitia huduma hii muhimu ya bima wakulima na wafugaji wanaweza kusaidiwa kupitia fidia pale mazao yao yanapokumbwa na majanga ya asili ikiwemo mvua ya mawe, mafuriko, majanga ya moto, na majanga mengine ya asili,’’ amesema Swilla.

Related Posts