KOCHA wa Maafande wa Polisi Tanzania, Bernard Fabian amesema ili timu hiyo ifanye vizuri na kutimiza adhima ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao, inahitaji sana mashabiki kujitokeza viwanjani kuwapa sapoti tofauti na wanavyofanya kwa sasa.
Timu hiyo iliyocheza michezo tisa kabla ya ule wa jana dhidi ya Maafande wenzao wa Green Warriors, imeshinda miwili tu, sare mitatu na kupoteza minne, jambo ambalo Fabian anaamini limechangiwa na muitikio mdogo wa mashabiki uwanjani kwao.
“Kwa michezo ya ugenini ni ngumu kwao kusafiri mara kwa mara ila kwa nyumbani ni muhimu sana kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao, hii itasaidia kuongeza morali ya wachezaji kupambana wakiamini wana watu wanaowapa motisha,” alisema.
Kocha huyo aliongeza, jambo kubwa ambalo wanalizingatia ni kuhakikisha wanaendelea kupata pointi, huku changamoto hizo wakiendelea kuzifanyia kazi siku baada ya siku, licha ya ushindani kuongezeka hasa michezo yao ya ugenini kwa msimu huu.
Fabian ambaye msimu uliopita alikuwa kocha msaidizi wa Tabora United, amejiunga na timu hiyo msimu huu akichukua nafasi ya John Tamba aliyeondoka, huku akipambania kukirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023.