Kuwa makini mitandao isikuvunjia ndoa yako

Tuanze na kisa kilichotokea nchini Marekani mwaka jana. Mwanandoa mmoja alimtoa roho mwenzie kisa mitandao ya kijamii na tamaa. Wanandoa hawa waliokuwa wamedumu miaka 10 walijikuta pakanga. Baba alipokea baruapepe toka kwa matapeli ikimtaarifu kuwa atarithi dola za Kimarekani milioni 30.

Naye bila kufanya ajizi, alimtaarifu mwenzake bahati hii ya kupata fedha ambayo hakuitolea jasho wala kutegemea. Taarifa hii iligeuka mauti kwa mume. Bibi tamaa ilimuwaka akaamua kumpa sumu ili arithi yeye utajiri huu wa ghafla bin vu.

Mwanamke alianza kuota matanuzi, tena akiwa pekee asijue mwishowe utakuwa majuto, dhambi, kosa la mauaji na kifungo cha miaka 25. Baada ya kuwa amemwekea sumu mumewe, mke alianza kuwasiliana na mtu (tapeli) aliyekuwa amemtumia baruapepe mumewe. Haukupita muda akagundua kuwa kumbe ile baruapepe ilikuwa kanyabwoya. Hakuwa na la kufanya, bali kumwibia siri shoga yake akiwa mwingi wa hasira, majuto, na simanzi kwa ukatili na upumbavu wake mbali na roho mbaya, tamaa, na ukatili. Maji yalikuwa yameishamwagika.

Hapa unajifunza nini? Mosi, si kila ving’aravyo ni dhahabu. Pili, majuto ni mjukuu. Na tatu, tamaa mbele mauti nyuma. Maskini kiumbe asiye na hatia alipoteza maisha yake bila kosa.

Kisa cha pili ni cha mama tajiri aliyefiwa na mumewe na kuamua kutafuta mwenza mtandaoni. Huyu mama alipata mtarajiwa aliyetokea kumpenda. Muda haukupita, wawili walikutana na wakaamua kuishi kama mke na mume. Kama kwenye kisa cha kwanza, kabla ya kukubali kuishi pamoja, mama alimwamini mwenzie na kumwambia kuwa alikuwa amerithi dola milioni saba za Kimarekani. Jamaa alipiga konde moyo na kuingia ndoa ya mashaka.

Haukupita muda baba akaamua kumuua yule mama ili arithi pesa hii nono. Baada ya mama kuwa amezikwa, kumbe kuna kitu alikuwa amemficha ambacho ni watoto wake wawili wa kiume ambao walikuwa ndio warithi wa fedha husika.

Kutokana na namna mama alivyouawa, watoto waliamua kuajiri mpelelezi aliyefumua kila kitu na kugundua ukweli kuwa kumbe yule baba alikuwa amemuua yule mwanamke aliyemwamini. Kufupisha kisa kirefu, jamaa alihukumiwa kifungo cha maisha bila msamaha.

Mara nyingi, ndoa nyingi zimeyumba, kuimarika au kuvunjika kutokana na wanandoa wanavyotumia mitandao ya kijamii, hasa simu na baruapeppe zao. Si ajabu kusikia malalamiko kuwa wanandoa hawawezi kupokea hata kugusa simu za wenzi wao.
Mwanandoa yeyote mwenye siri zake na mambo yake yasiyofaa, hawezi kumpa nywila ya simu yake mwenzake. Hii ni kutaka kuficha mambo yake ya hovyo. Hata hivyo, kila lenye mwanzo lina mwisho. Wengi wanaofanya hujikuta wakijuta baada ya kuwakosa wale waliowahitaji.
Pamoja na kwamba haya mambo yapo, yupo mmoja aliyewashangaza hata kuwahuzunisha watoto wake. Siku moja aliingia maliwatoni kuoga. Bahati mbaya alisahau simu yake chumbani. Mara simu ikaita. Wakati ikiita, alisikia, bila kujali, alichomoka maliwatoni kuwahi simu. Mkewe hakuwa akimshuku kwa lolote. Hivyo, aliamua kuinyakua simu na kuipokea.
Mara sauti ya kike ikasikika ikisema “darling mbona unachelewa kupokea simu?” Yule mama hakufanya papara. Alimtaka mumewe apokee simu. Mume aliikata. Mama alikubali yaishe japo hayakuisha. Alikwenda kwa wataalamu wa mitandao wakamfundisha jinsi ya kuidukua ile simu. Baada ya kupata ushahidi wa kutosha, mama alichukua zile taarifa na kuzinakili kwenye simu yake. Siku isiyo jina si alimtolea baba kila kitu. Baba alijikuta kanaswa na tundu bovu kiasi cha kuadhirika na kusababisha ufa kwenye ndoa yake.

Related Posts