MSHIKEMSHIKE wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa 12 unaendelea leo kwa kuchezwa mechi tatu za kibabe na zilizobeba rekodi.
Mchezo wa kwanza utakuwa saa 10:00 jioni na JKT Tanzania iliyopo nafasi ya 11 kabla ya mechi za jana na pointi zake 10, itaikaribisha Tanzania Prisons ilio nafasi ya 12 na pointi 10.
Mchezo huu unaowakutanisha maafande wote kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo umekaa kimtego kwani atakayeshinda atamzidi mwenzake pointi tatu kutokana na hivi sasa zipo sawa.
Timu hizo zinakutana huku JKT ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia pointi nne kwenye mechi tano za mwisho ikipata sare moja na kushinda moja huku ikipoteza mechi mbili.
Kwa upande wa Prisons, mechi tano za mwisho imeondoka na pointi tatu baada ya kushinda moja na kupoteza nne.
Mbali na hivyo, Prisons imekuwa na matokeo mazuri mbele ya JKT katika mechi tano za mwisho kutokana na kushinda mbili na sare tatu, haijapoteza iwe nyumbani au ugenini.
JKT ina kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wa leo kuondoa rekodi hiyo mbovu dhidi ya Prisons.
Kocha wa JKT, Ahmad Ally ametamba kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya huku akibainisha hawana cha kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani.
“Tutaingia kwa kumheshimu mpinzani wetu, tunaamini hautakuwa mchezo rahisi kutokana kila timu kuhitaji matokeo mazuri lakini kwa upande wetu maandalizi yamekwenda vizuri na wachezaji wapo kwenye hali nzuri,” alisema.
Kocha wa Prisons, Mbwana Makata alisema ni mchezo muhimu kwao na wanahitaji pointi tatu ili kuendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya nafasi kwenye msimamo.
TABORA UNITED VS SINGIDA BS
Mchezo huu utaanza saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora na wenyeji Tabora United waliotoka kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Yanga, watapambana na Singida Black Stars ambayo haijaonja ladha ya ushindi katika michezo miwili ya mwisho ikiambulia kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga na suluhu dhidi ya Coastal Union.
Wakati ikiwa na rekodi hiyo mbaya, Singida Black Stars mechi mbili za mwisho ugenini imeshinda zote, hivyo leo Tabora United wanapaswa kuwa makini licha ya kwamba nao nyumbani wapo vizuri wakishinda mechi mbili za mwisho.
Tabora United iliyokuwa nafasi ya sita na pointi 17 baada ya michezo 10, inahitaji ushindi ili kujisogeza nafasi za juu wakati wenzao Singida Black Stars iliyopo nafasi ya tatu na pointi 23 kabla ya mechi za jana ikishinda itakuwa nafasi nzuri ya wao kuishusha Yanga na kukamata nafasi ya pili.
Siku itahitimishwa kwa mchezo kati ya Dodoma Jiji dhidi ya KMC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Wenyeji Dodoma Jiji waliopo nafasi ya 9 na pointi 13 kabla ya mechi za jana, wana kumbukumbu ya kuifunga KMC bao 1-0 katika mchezo wa mwisho waliokutana msimu uliopita.
Kumbukumbu mbaya kwa timu zote ni, mechi za mwisho kabla ya ligi kusimama msimu huu walipoteza, JKT Tanzania ikifungwa 2-1 na Kagera Sugar, wakati KMC ikichapwa na Simba 4-0.
Mchezo huo utakaopigwa saa 1:00 usiku, Dodoma Jiji wanaingia kifua mbele wakiwa na rekodi ya kufanya vizuri wanapokuwa nyumbani kwani mechi nne za mwisho wameshinda tatu na kupoteza moja, huku KMC mechi nne za mwisho ugenini wakishinda moja na kupoteza tatu.