Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imemsimamisha Esther Fredrick, mke wa Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Fredrick Sumaye kutekeleza tuzo iliyotolewa na Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi iliyompa ushindi katika kesi ya mgogoro wa umiliki wa shamba lililokuwa linabishaniwa.
Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi ilimtangaza Mama Sumaye kuwa mmiliki halali wa shamba hilo namba 25 la hekta 1.690, lililoko Madale Wazo Hill, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, lenye hati namba 53085.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Zephrine Galeba, imesimamisha utekelezaji wa tuzo ya hukumu hiyo, kufuatia shauri la maombi ya kusimamisha utekelezaji huo, lililofunguliwa na mshindwa tuzo katika kesi hiyo ya msingi, Jimmy Mushi.
Katika shauri hilo la maombi ya madai namba 902/2024, Mushi aliiomba Mahakama hiyo itoe amri ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu na tuzo ya Mahakama Kuu kusubiri uamuzi wa rufaa anayokusudia kuikata.
Hata hivyo, Wakili wa Mushi, Mashaka Mfala alipoulizwa na Mwananchi leo Jumapili, Novemba 24, 2024 iwapo wameshakata rufaa hiyo, hakutaka kuizungumzia akidai hawezi kutoka taarifa za mteja wake bila ridhaa yake.
Ingawa Mushi alikuwa tayari kutoa dhamana ya benki yenye thamani Sh60 milioni, ili kutekeleza matakwa ya kanuni za Mahakama hiyo, lakini Jaji Galeba ameikataa dhamana hiyo akisema aina ya tuzo inayoombwa kusimamishwa utekelezaji wake hastahili kuwekewa dhamana hiyo.
Badala yake amekubaliana na maombi hayo ya Mushi kusimamisha mchakato wa utekelezaji wa tuzo hiyo kwa masharti pekee ambayo Mushi anatakiwa kuzingatia.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo wakili wa Mushi, Mashaka Mfala aliieleza Mahakama kuwa, mteja wake amekidhi matakwa ya kikanuni, kwa mujibu wa kanuni ya 11 (4), (5) na (7) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka 2009 (the Rules).
Amesema kwa kuzingatia matakwa ya kanuni ya 11 (5) (b), mteja wake yuko tayari kutoa dhamana ya kibenki yenye thamani ya Sh60 milioni kiasi ambacho makadirio ya thamani ya nyumba na uwiano wa ardhi hiyo.
Mawakili wa Mama Sumaye, Emmanuel Saghan na Elly Mkwawa, walitaka Mushi atoe dhamana ya benki yenye thamani ya Sh500 milioni ambazo amesema zilikuwa thamani ya mwisho ya shamba lote husika.
Hata hivyo, Jaji Galeba katika uamuzi wake, alioutoa Novemba 5, 2024, amesema tuzo hiyo haihusishi malipo ya fedha maalumu kwa mshinda tuzo bali amri ya kuondolewa kwa mshindwa tuzo.
Amesema usimamishwaji na utekelezaji wa tuzo ya aina hiyo, ni mtizamo wake kuwa hauwezi kuhitaji kuwekewa dhamana ya pesa au dhamana ya benki, kwa kuzingatia kanuni ya 11 (5) (b) ya Kanuni ya Mahakama ya Rufani, namna ilivyowekwa.
“Hivyo sina msingi wowote wa kuamuru mwombaji (Mushi) kufanya mchakato wa dhamana ya benki, katika mazingira ya hii kesi. Ningefanya hivyo kwa urahisi kama utekelezaji wa tuzo ingekuwa wa malipo ya fedha”, amesema Jaji Galeba.
Hata hivyo, Jaji Galeba amesema bila kuzingatia hayo, Mahakama hiyo bado ina mamlaka ya chini ya kanuni ya 11(3) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa, kusimamisha utekelezaji wa tuzo inayobishaniwa, kwa kuweka masharti yanayofaa, yatakayopaswa kutekelezwa na mwombaji, kwa kadri iwezekanavyo.
Jaji Galeba amebainisha lengo la kuweka masharti hayo ni kulinda na kuhifadhi haki za mujibu maombi (Mama Sumaye) ambaye ana hukumu halali inayomnufaisha.
“Kwa kuzingatia mjadala huo hapo juu, hasa kwa kuzingatia asili ya tuzo, ambayo inampa mjibu maombi (Mama Sumaye) amri ya kuhamisha (mshindwa tuzo, Mushi), ninatoa amri zifuatazo”, amesema Jaji Galeba na kuamuru:
“Mchakato wote wa tuzo ya Aprili 25, 2023 kati ya wadaiwa katika haya maombi, inasimamishwa kusubiri uamuzi wa rufaa inayokusudiwa kukatwa, kutegemeana na masharti yafuatayo kufuatwa kikamilifu na mwombaji.”
Katika masharti hayo Jaji Galeba ameamuru kuwa Mushi hataliachia shamba hilo na kwamba kama atataka kuliachia wakati wowote basi itabidi amkabidhi Mama Sumaye.
Pia, Jaji Galeba ameamuru kuwa Mushi hataliuza shamba hilo, kulipangisha, kuingia katika ubia wala kufanya kitendo chochote kitakachohusisha masilahi ya upande wa tatu.
Vilevile ameamuru kuwa ikiwa shamba hilo litabaki wazi yaani kama mwombaji Mushi atadhihirika kutokuwamo ndani ya shamba hilo kwa kipindi cha zaidi ya siku 90, mjibu maombi, Mama Sumaye atachukua umiliki wa shamba hilo.
Mwisho Jaji Galeba ameamuru kuwa kwa muda wote huo ambao shamba hilo litabakia kuwa katika himaya ya Mushi, kabla ya rufaa yake kuamuriwa, ataendelea (Mushi) kulilipia kodi zote za Serikali au Serikali za mitaa, kwa jina la mjibu maombi, Mama Sumaye.
Kesi ya msingi ilifunguliwa na Esther Fredrick Sumaye dhidi ya Jimmy Peter Mushi.
Katika kesi hiyo ya ardhi namba 99/2023, Mama Sumaye alikuwa alimlalamikia Mushi kuwa alikuwa amevamia shamba lake hilo.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda Aprili 25, 2024, ilimtangaza Mama Sumaye kuwa mmiliki halali wa shamba hilo.
Mushi hakuridhika na hukumu hiyo, hivyo aliwasilisha notisi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Kabla kukamilisha hatua ya kukata rufaa, kuwasilisha sababu za rufaa, Mama Sumaye akaanza mchakato wa utekelezaji wa tuzo yake kwa lengo la kumuondoa Mushi katika shamba hilo, ndipo akafungua shauri hilo la maombi ya kusimamisha utekelezaji wa tuzo hiyo.